Qalibaf: Iran italipiza kisasi damu ya Kiongozi Shahidi
-
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, ameahidi kwamba Jamhuri ya Kiislamu haitaruhusu damu ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyeuawa shahidi, Ayatollah Sayyid Ali Khamenei, na mashahidi wengine wa uvamizi wa Marekani na Israel dhidi ya taifa hili “kupotea bila kulipiziwa kisasi.”
Kiongozi huyo wa ngazi ya juu ametoa kauli hizo siku ya Jumanne, akiwaenzi wahanga 168, wengi wao wakiwa wanafunzi wa shule, waliouawa kwa kulengwa katika shule ya Shajara Tayyiba mjini Minab, kusini mwa Iran, wakati wa siku ya kwanza vya vita vya kichokozi vya Marekani na Israel dhidi Iran vilivyoanza tarehe 28 Februari na kuendelea hadi 7 Aprili.
Qalibaf ameapa kwamba, chini ya uongozi wa mwana na mrithi wa Shahidi Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei, Jamhuri ya Kiislamu “itaelekeza uwezo wake wote katika kulinda haki za watu wa Iran, kukomesha uvamizi, kumuadhibu mvamizi, na kudumisha heshima na msimamo wa nchi.”
Ameongeza kuwa: “Hatutaruhusu adui kulenga umoja wetu wa kitaifa, ushiriki wa wananchi [katika kuunga mkono Jamhuri ya Kiislamu], ustahimilivu wa taifa, au motisha ya maafisa wetu.”
Aidha amesema, kwa kunufaika na miongozo iliyotolewa na Ayatullah Mojtaba Khamenei, taifa litaibuka mshindi kutoka katika mtihani huu wa kihistoria na kupewa ushindi wa kiungu.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Qalibaf amesisitiza kuwa Iran haitafungua Lango Bahari la Hormuz, ambao imelifunga kama jibu la uvamizi wa kigeni, hadi pale Marekani itakapondoa mzingiro wa baharini iliyouwekea Jamhuri ya Kiislamu.
Aidha amesema kufunguliwa kwa lango bahari hilo pia kunategemea kuachiliwa kwa mali za nchi zilizozuiwa , kuondolewa kwa vikwazo haramu vya mafuta, na kusitishwa kwa vitisho vya kijeshi na uvamizi katika nyanja zote, pamoja na kutekelezwa kwa masharti mengine yote yaliyomo katika mkataba wa maelewano uliotiwa saini kati ya Iran na Marekani mwezi Juni.
Ameutaja mkataba huo wa maelewano kama “nyaraka ya kushindwa kwa Marekani katika nyanja za kisheria na kisiasa.”
Amesema adui alikubali mkataba huo “kwa kukata tamaa ili kuhitimisha vita.” Aidha amesema majibu madhubuti na yenye mafanikio ya Iran dhidi ya uvamizi yalilazimisha Washington kutangaza usitishaji vita wa upande mmoja mnamo Aprili 7 na kisha kukubaliana na maelewano hayo.