Hichilema ashinda uchaguzi wa rais wa Zambia kwa asilimia 60 ya kura
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140754-hichilema_ashinda_uchaguzi_wa_rais_wa_zambia_kwa_asilimia_60_ya_kura
Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, ameshinda uchaguzi mkuu wa nchi hiyo kwa takriban asilimia 60 ya kura zilizopigwa wiki iliyopita. Hayo yametangazwa mapema leo Jumanne na Tume ya Uchaguzi ya Zambia.
(last modified 2026-08-18T09:18:28+00:00 )
Aug 18, 2026 03:23 UTC
  • Hakainde Hichilema
    Hakainde Hichilema

Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, ameshinda uchaguzi mkuu wa nchi hiyo kwa takriban asilimia 60 ya kura zilizopigwa wiki iliyopita. Hayo yametangazwa mapema leo Jumanne na Tume ya Uchaguzi ya Zambia.

Matokeo hayo yalitarajiwa sana, huku Hichilema, akiwa madarakani tangu 2021, akikabiliana na wagombea 13 wakiongozwa na waziri wa zamani wa majimbo, Brian Mundubile, wa chama cha upinzani cha National Reconciliation Party for Unity and Prosperity (NRPUP), akijaribu kwa mara ya kwanza kuwania urais.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zambia, Mwangala Zaloumis amesema Mundubile, 55, ambaye aliingia katika kinyang'anyiro hicho mwezi Mei, amepata karibu asilimia 38 ya kura.

Amesema kura za majimbo matano kati ya 226 ya uchaguzi hazikuwa zimehesabiwa. Hata hivyo, "matokeo ya majimbo hayo hayawezi kuathiri matokeo jumla ya uchaguzi huo," amesisitiza Mwangala Zaloumis.

Uchaguzi wa Agosti 13 katika taifa hilo lenye utajiri wa madini ya shaba kusini mwa Afrika, uligubikwa na madai ya udanganyifu na kusimamishwa zoezi la kuhesabiwa kura nchini kote baada ya mashambulizi dhidi ya maafisa wa zoezi la uchaguzi na wizi wa karatasi za kupigia kura.

Kabla ya uchaguzi huo, vyama vya upinzani na makundi ya asasi za kiraia yalionya kuhusu mbinyo wa kisiasa, yakitaja vikwazo vilivyowekwa na serikali dhidi ya kampeni za uchaguzi za kambi ya upinzani.

Uchaguzi wa rais wa Zambia ulionekana kama kura ya maoni kuhusu muhula wa kwanza wa Hichilema ambapo uchumi wa Zambia ulirejea katika mkondo wa ustawi baada ya miaka mingi ya matatizo ya kifedha.