Namna Dunia Inavyorejea katika Enzi za Ukatili na Ufedhuli?
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema karibuni hivi kwamba "matumizi ya nguvu za wazi na madai ya kumiliki rasilimali za mataifa mengine ni ishara zinazoonyesha kuwa tunarejea kwenye zama za kale za matumizi ya nguvu, ambalo lilikuwa jambo la kawaida na lisilodhibitiwa."
Onyo hili la Esmaeil Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, linatoa taswira ya kutia wasiwasi kuhusu hali ya sasa ya mfumo wa kimataifa, ambao ulibuniwa baada ya vita viwili vikuu vya dunia na uzoefu mchungu wa ukoloni, ukiegemea misingi ya Hati ya Umoja wa Mataifa, mamlaka ya mataifa kujitawala, marufuku ya matumizi ya nguvu, na kulinda haki za kibinadamu, lakini ambao sasa umeporomoka kutokana na mashinikizo ya siasa za mabavu, undumakuwili na udhaifu wa taasisi za kimataifa.
Kauli ya Baghaei imetolewa katika muktadha wa jinai za kivita zilizofanywa hivi karibuni na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni wa Israel, hususan matukio yaliyotokea katika miji ya Iran ya Minab na Lamerd ambayo taathira zake zinavuka mipaka ya janga la kitaifa. Ni wazi kuwa kama mashambulizi ya kigaidi katika maeneo ya raia, vitisho kwa miundombinu muhimu na ukiukwaji wa sheria za kibinadamu vitaachwa bila kuadhibiwa, matokeo yake yatakuwa ni dhulma dhidi ya wahanga, na sheria kutokuwa na maana tena katika mahusiano ya kimataifa.
Mgogoro wa Palestina ni mfano wa wazi zaidi kuhusu suala hili. Akiangazia vita na mauaji ya kimbari yanayoendelea huko Palestina pamoja na ukatili unaoshuhudiwa Lebanon, Baghaei anaona utendaji dhaifu wa Umoja wa Mataifa kama ishara ya "kuporomoka kwa kasi hadhi na itibari" ya taasisi hiyo. Ukosoaji huu unajikita katika hoja ya msingi kwamba taasisi ambayo lengo lake kuu ni kudumisha amani na kuzuia vita hupoteza hadhi yake pale inaposhindwa kuchukua hatua madhubuti mbele ya ukiukwaji wa wazi wa hati yake, na badala yake kujaribu kuweka uwiano bandia kati ya mchokozi na mwathirika, au kuridhika tu kwa kutoa taarifa zisizo na mifumo ya utekelezaji.
Bila shaka, tatizo si udhaifu wa taasisi moja pekee. Mgogoro wa kina zaidi unatokana na pengo lililopo kati ya kanuni za kimataifa na jinsi zinavyotekelezwa kwa upendeleo. Sheria za kimataifa huwa na maana pale tu kanuni zake zinapozingatiwa na kutekelezwa kwa usawa na mataifa makubwa na madogo, pamoja na washirika na wapinzani wao. Wakati nchi moja inapowekewa vikwazo na mashinikizo kwa madai ya kukiuka sheria, na nyingine kukiuka hadharani sheria hizohizo kwa kutegemea nguvu zake za kisiasa na kijeshi, na kisha kutochukuliwa hatua yoyote, ujumbe wa wazi huwa umetumwa kwa ulimwengu kwamba nguvu inaweza kuchukua nafasi ya sheria.
Kwa mtazamo huu, onyo la Baghaei kuhusu vitisho dhidi ya maeneo ya raia linapata uzito wa ziada. Sheria ya kimataifa ya kibinadamu ni matokeo ya juhudi za karne nzima za kudhibiti ukatili wa vita, ikiwa ni mkusanyiko wa kanuni zilizoundwa ili kuwalinda raia, majeruhi na wale wasioshiriki katika mapigano. Kupuuzwa waziwazi kanuni hizi kunaashiria kurejea kwa mantiki ya vita visivyodhibitiwa, ambapo nguvu ya kijeshi ndiyo huamua mipaka inayokubalika ya matumizi ya nguvu na ukatili.
Baghaei analinganisha hali hii na uzoefu wa ukoloni wa jadi ambapo uporaji wa ardhi, unyang'anyi wa rasilimali na kulazimishwa mataifa dhaifu kufuata matakwa ya mataifa yenye nguvu duniani vilikuwa sehemu muhimu ya mahusiano ya kimataifa. Ingawa sura ya ukoloni imebadilika leo, lakini kama mataifa yenye nguvu yataruhusiwa kufikia malengo yao ya kisiasa au kupora rasilimali za mataifa mengine na suala hilo kufanywa kuwa jambo la kawaida, hakutakuwepo tena na tofauti kubwa kati ya mfumo wa sasa wa kisheria na mienendo ya nguvu ya zama za ukoloni.
Maonyo kuhusu hatima ya Umoja wa Mataifa pia yanapaswa kutazamwa katika muktadha huu. Jumuiya ya Mataifa (League of Nations) haikuanguka kutokana na tukio moja la ghafla, bali hadhi na uaminifu wake vilitoweka taratibu kutokana na mfululizo wa changamoto, kushindwa kuzuia vitendo vya uchokozi, na ukosefu wa imani miongoni mwa mataifa yenye nguvu kuhusu uwezo wake wa kusimamia utekelezaji wa sheria. Ingawa Umoja wa Mataifa leo bado umesimama imara kimaundo, lakini kushindwa kwake mara kwa mara kushughulikia migogoro mikubwa ya kimataifa kunahatarisha kuugeuza kuwa taasisi inayodumisha taswira ya utulivu kwa nje huku ikipoteza uwezo wake wa kutekeleza majukumu yake inavyotakiwa.
Katika muktadha huo, suala la msingi si hatima ya Umoja wa Mataifa pekee, bali ni hatima ya mfumo wa dunia nzima. Iwapo sheria ya mamlaka ya kujitawala kwa mataifa itadhoofishwa, uhuru wa mipaka ya nchi kuwekwa chini ya nguvu za kijeshi, na sheria za kibinadamu kulazimishwa kupisha maslahi ya kisiasa ya mataifa makubwa, dunia itaingia katika zama ambazo mataifa ya ukubwa wa wastani au madogo hayataweza kutegemea tena ulinzi wa kisheria kwa ajili ya usalama wao.
Kwa mtazamo huo, wito wa Baghaei wa "kulindwa maadili na kanuni zote ambazo ustaarabu wa mwanadamu umefikia katika kipindi cha karne nyingi" unatoa ujumbe unaovuka mipaka ya migogoro mahususi inayohusisha Iran, Marekani na utawala wa Kizayuni. Kulinda mamlaka ya kitaifa, uhuru wa kisiasa, umoja wa mipaka ya nchi, na utu wa binadamu kuna maana tu ikiwa kanuni hizi zitasalia kuwa za kimataifa na zinazotekelezwa kwa usawa kwa wote. Kuzilinda si suala la nchi moja kusimama dhidi ya nyingine; bali ni kulinda kanuni yenyewe inayolenga kuwezesha mataifa kuishi pamoja kwa amani.
Hapa ndipo hasa penye hatari kubwa zaidi. Mfumo wa kimataifa hauporomoki kwa sababu tu Umoja wa Mataifa umeshindwa kufanya kazi, huporomoka pale nchi zenye nguvu zinapochukua nafasi ya sheria na dunia kulazimishwa kuzoea hali hiyo. Ikiwa mwenendo wa sasa utaendelea, suala hili si tu litarejesha tena mgogoro wa kikanda, bali dunia nzima inaweza kurejea tena katika zama ambapo nguvu na mabavu ndiyo yatakuwa na uhalali, na usalama kunyimwa nafasi ya kudhamini usalama wa wanyonge.