Rais wa Zambia aahidi kukuza uchumi baada ya kushinda uchaguzi
-
Rais Hakainde Hichilema wa Zambia
Rais Hakainde Hichilema wa Zambia amesema kuwa atatumia muhula wake mpya kukuza uchumi wa nchi hiyo na kuandaa fursa zaidi kwa wananchi ili kupunguza gharama za maisha.
Katika hotuba yake ya kwanza kwa taifa baada ya kuchaguliwa tena kwa ushindi mkubwa baada ya kutangazwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa rais katika mji mkuu wa Zambia, Lusaka, Hichilema amesema kuwa hatapuuza uungaji mkono na imani iliyoonyeshwa na wananchi wa Zambia kwake
Zambia ni miongoni mwa nchi wazalishaji wakuu wa madini ya shaba barani Afrika.
“Maendeleo yatafika kwa kila jamii na kaya. Wananchi wa Zambia kwa mara nyingine tena wametukabidhi jukumu kubwa zaidi ambalo raia wanaweza kumtwika kiongozi wao. Tunalipokea jukumu hilo kwa unyenyekevu, na hatutalipuuza wala kulitumia vibaya,” amesema Hakainde Hichilema katika hotuba kwa njia ya televisheni kutoka makazi yake, jijini Lusaka.
Tume ya uchaguzi ya Zambia ilimtangaza Hichilema kuwa Rais mteule baada ya kupata kura milioni 2.9, ikilinganishwa na kura milioni 1.8 alizopata mpinzani wake mkuu, Brian Mundubile wa chama cha National Restoration Party for Unity and Progress.
Vyombo vya habari vya Zambia vimeripoti kuwa Mundubile anachunguza hatua za kisheria za kupinga matokeo hayo ya uchaguzi.
Hichilema mwenye umri wa miaka 64, ambaye ni mchumi na mfugaji, aligombea kwa tiketi ya chama tawala cha United Party for National Development. Alishinda muhula wake wa kwanza kwa tofauti ya zaidi ya kura milioni moja baada ya kumtimulia kivumbi Rais wa wakati huo, Edgar Lungu.
Hichilema ameeleza kuwa mshindi mkuu wa uchaguzi huo ni watu wa Zambia wenye asili na tamaduni mbalimbali wapatao milioni 21; ambao amesema wana uwezo wa kuchangia katika mustakabali wa uchumi wa nchi hiyo.