Iran yawatimua wanadiplomasia wawili wa Ufaransa kutokana na mienendo yao haramu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140794-iran_yawatimua_wanadiplomasia_wawili_wa_ufaransa_kutokana_na_mienendo_yao_haramu
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imewatangaza wanadiplomasia wawili wa Ufaransa wanaofanya kazi katika Ubalozi wa Ufaransa mjini Tehran kuwa ni watu wasiostahili kutokana na shughuli zao zinazotambuliwa kuwa kinyume na sheria za kimataifa na Mkataba wa Vienna wa 1961 kuhusu Mahusiano ya Kidiplomasia.
(last modified 2026-08-19T10:07:50+00:00 )
Aug 19, 2026 10:05 UTC
  • Wizara ya Mambo ya Nje Iran
    Wizara ya Mambo ya Nje Iran

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imewatangaza wanadiplomasia wawili wa Ufaransa wanaofanya kazi katika Ubalozi wa Ufaransa mjini Tehran kuwa ni watu wasiostahili kutokana na shughuli zao zinazotambuliwa kuwa kinyume na sheria za kimataifa na Mkataba wa Vienna wa 1961 kuhusu Mahusiano ya Kidiplomasia.

Katika taarifa iliyotolewa usiku wa kuamkia leo Jumatano, Ofisi ya Mahusiano ya Umma ya wizara hiyo ilisema maafisa hao wawili wa Ufaransa walishiriki katika shughuli zinazokiuka sheria za kimataifa, hasa vifungu vya Mkataba wa Vienna wa 1961.

Taarifa hiyo imesema kwamba licha ya wiki kadhaa kupita tangu mwenendo wao haramu ufichuliwe, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na serikali ya Ufaransa kurekebisha tabia zao au kutoa hakikisho kwamba mwenendo huo hautarudiwa.

"Kwa hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje inawatambua maafisa hawa wawili kama watu wasiostahili, na kuanzia sasa wanapigwa marufuku kuingia Iran," imesema taarifa hiyo.

Mwezi Julai mwaka huu 2026, wanadiplomasia hao wawili wa Ufaransa walikamatwa kwa muda mjini Tehran baada ya kupatikana kwenye mkutano uliohusishwa na uchunguzi wa usalama.

Ufaransa iliwashutumu askari usalama wa Iran kuwa wamewatendea vibaya wanadiplomasia hao, lakini Tehran ilipinga madai hayo na kusema kwamba wamehojiwa kuhusu mwenendo "usio wa kawaida".

Wizara ya Intelijensia ya Iran imesema wanadiplomasia hao wawili walikuwa na "rekodi nyingi za ukiukaji wa sheria za ndani na majukumu yao ya kidiplomasia."

Baada ya utambulisho wao kuthibitishwa, suala hilo liliripotiwa Wizara ya Mambo ya Nje, na wanadiplomasia hao walikabidhiwa kwa balozi wa Iran nchini Ufaransa mbele ya polisi wa kidiplomasia.

Wizara hiyo imesema, baadaye Ufaransa ilizindua kampeni ya vyombo vya habari yenye lengo la kupotosha fikra za umma kuhusu ukiukwaji huo wa sheria, ikisema uchunguzi wa awali wa nyaraka zilizopatikana katika eneo hilo ulifichua mradi unaohusisha uingiliaji kati wa kigeni katika masuala ya ndani.

Siku ya Jumatatu iliyopita, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei alisema serikali ilitarajia maafisa wa Ufaransa kuomba msamaha kutokana na tukio hilo, akieleza kuwa maafisa wa Ufaransa wenyewe walikuwa wamekiri kwamba watu hao wawili si wanadiplomasia bali walikuwa mawakala.

"Hili lenyewe ni kukiri kwamba Mkataba wa Vienna umekiukwa," alisema Esmaeil Baqaei.