Araghchi: Nchi za Kiislamu ziwajibike kupinga kukiukwa mamlaka ya kujitawala Iran
-
Hissein Brahim Taha and Abbas Araqhchi
Katika mazungumzo ya simu na Katibu Mkuu Mpya wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amessitiza umuhimu wa nchi za Kiislamu kuwajibika ipasavyo kupinga kukiukwa mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi nzima ya Iran na wakati huo huo kukabiliana na matumizi ya nguvu na hujuma za uvamizi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa anatumai kuwa Katibu Mkuu huyo Mpya atatumia vyema uwezo wa jumuiya ya OIC kuimarisha umoja na uratibu miongoni mwa mataifa ya Kiislamu katika kushughulikia matukio na changamoto zinazoukabili Ulimwengu Kiislamu.
Sayyid Abbas Araghchi amebainisha haya wakati akimpongeza Hissein Brahim Taha kwa kuteuliwa kwake kuwa Katibu Mkuu Mpya wa Jumuiya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na kumtakia mafanikio katika wadhifa wake mpya.
Katika mazungumzo hayo, Araghchi amemweleza Katibu Mkuu wa OIC kuhusu matukio ya hivi karibuni ya kikanda kufuatia uchokozi uliofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, na kusisitiza kuwa kuna umuhimu mataifa ya Kiislamu kuchukua hatua madhubuti za uwajibikaji kupinga kukiukwa mamlaka ya kujitawala wa umoja wa ardhi nzima ya Iran.
"Mataifa ya Kiislamu yanapasa kuwajibika ipasavyo kukabiliana na matumizi ya nguvu na vitendo vya uchokozi," amesisitiza Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.