Araqchi: Iran haitaki vita, lakini iko tayari kuendelea kujilinda ikilazimu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i138902-araqchi_iran_haitaki_vita_lakini_iko_tayari_kuendelea_kujilinda_ikilazimu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema Iran haitaki vita, lakini iko tayari kuendelea kujilinda inapobidi.
(last modified 2026-06-05T03:08:09+00:00 )
Jun 05, 2026 03:05 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika mahojiano na al Mayadeen
    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika mahojiano na al Mayadeen

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema Iran haitaki vita, lakini iko tayari kuendelea kujilinda inapobidi.

"Hatujawahi kutaka vita. Tunataka amani, lakini amani ya heshima," amesema mwanadiplomasia mkuu wa Iran katika mahojiano yake na mtandao wa al-Mayadeen wa Lebanon jana Jumatano.

Hata hivyo, aliongeza, "Tuko tayari kuendelea na vita, iwe kwa upande wa uwezo wa kijeshi, mshikamano wa kitaifa au azma ya kukabiliana na uchokozi."

"Nafasi yetu ya kijeshi ni imara zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya vita, kwani tumeweza kudumisha uzalishaji wa zana za kijeshi katika kipindi chote cha vita, na hawakuweza kuusimamisha," ameongeza Sayyid Abbas Araqchi, akimaanisha uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran ulianzia Februari 28 hadi Aprili 7.

"Kwa hivyo, tuna uwezo wa kuendelea na vita kwa muda mrefu kadiri iwezekanavyo."

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza kuwa, "Ikiwa mantiki itashinda, vita havitaendelea tena."

Araqchi amesema kwamba uchokozi wa hivi karibuni umebadilisha mitazamo ya Wamarekani kuhusu nguvu ya Iran.

"Wamarekani, katika vita vya hivi karibuni, walielewa vyema nguvu halisi ya Iran," amesema na kuongeza: Washington haikutimiza malengo yake, ikiwa ni pamoja na takwa lake la awali la "kujisalimisha Iran bila masharti".

Wakati huo huo, Araghchi ameashiria msisitizo wa Iran wa kukomesha uchokozi katika pande zote, ikiwa ni pamoja na Lebanon, kama sharti la lazima la Jamhuri ya Kiislamu na kama sehemu ya makubaliano yoyote tarajiwa na Marekani.

"Hatuoni hatima ya vita kati ya Iran na Marekani na Israel kuwa tofauti na hatima ya vita vya Lebanon," amesema Sayyid Araqchi. Ameongeza: "Vita vitaisha katika sehemu zote mbili (Iran na Lebanon), au vinaendelea katika sehemu zote mbili."