Duru za kuaminika: Saudia imepinga Misri kuingizwa kwenye Makubaliano ya Makka
Saudi Arabia ilipinga Misri kujiunga na Mkataba wa Pamoja wa Ulinzi wa Makka uliosainiwa na Saudia, Uturuki na Pakistan wiki iliyopita, licha ya Ankara kutoa msukumo wa Cairo kujumuishwa kwenye mkataba huo. Hayo yameripotiwa na vyanzo vitatu vya Saudi Arabia vyenye taarifa za majadiliano yaliyofanywa juu ya suala hilo.
Mmoja wa vyanzo hivyo, ambaye ni mshauri mwandamizi wa zamani wa ufalme wa Saudia amesema, Riyadh haikutaka Misri ijiunge na makubaliano hayo "japo kwa hivi sasa".
Hata hivyo, vyanzo vyote vitatu, vilivyozungumza kwa sharti la kutotajwa majina kutokana na hali nyeti ya suala hilo, vimesema msimamo wa Saudi Arabia umechochewa na namna nchi hiyo inavyozidi kukatishwa tamaa na serikali ya Rais Abdel Fattah el-Sisi na imani iliyojengeka huko Riyadh kwamba Misri haina tena thamani na umuhimu wa kimkakati au kijeshi iliokuwa nao hapo kabla.
Mkataba wa Pamoja wa Ulinzi wa Makka, ambao ulisainiwa katika mji huo Mtakatifu wa Kiislamu siku ya Ijumaa iliyopita, unazitaka Saudi Arabia, Uturuki na Pakistan zichukulie shambulio la kijeshi dhidi ya yoyote kati ya nchi hizo, kuwa ni sawa na kuzishambulia nchi zote hizo tatu.
Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa, uamuzi wa Saudia wa kupinga kuingizwa Misri kwenye makubaliano ya Makka umetokana na mivutano inayoongezeka kati ya Riyadh na Cairo.
Vyanzo hivyo vinasema, Saudi Arabia ilikuwa mfadhili mkubwa wa kifedha wa serikali ya Sisi baada ya kunyakua madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi ya 2013, ambapo kwa kuanzia, Riyadh ilitumia karibu dola bilioni 25 kuinua hali ya uchumi wa Cairo uliokuwa umedorora, lakini ilikatishwa tamaa na kile ilichokiona kama kukosekana usaidizi na uungaji mkono wa mkabala kutoka upande wa Misri katika masuala nyeti ya usalama.
Moja ya vyanzo hivyo kimeashiria kile kilichoelezwa kama mchango "mdogo na usioaminika" wa Misri katika vita vya muda mrefu vya Saudia dhidi ya Wahouthi wa Yemen na msimamo wa kuvunja moyo wa Cairo wakati wa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Aidha, vyanzo vimeashiria wasiwasi wa Riyadh juu ya kile ilichokiona kama "utiifu" wa Cairo kwa Muungano wa Falme za Kiarabu, UAE hususan baada ya mzozo uliozuka kati ya Riyadh na Abu Dhabi kuhusu usaidizi wa Imarati kwa makundi yanayopigania kujitenga ya Kusini mwa Yemen ambayo yanaelezewa kuwa "yanatishia usalama na maslahi ya taifa ya Saudia"…/