Sababu na Umuhimu wa Makubaliano ya Makka
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140610-sababu_na_umuhimu_wa_makubaliano_ya_makka
Siku ya Ijumaa, Saudi Arabia, Uturuki na Pakistan zilitia saini "Makubaliano ya Makka ya Ulinzi wa Pamoja".
(last modified 2026-08-12T06:51:05+00:00 )
Aug 12, 2026 06:39 UTC
  • Sababu na Umuhimu wa Makubaliano ya Makka

Siku ya Ijumaa, Saudi Arabia, Uturuki na Pakistan zilitia saini "Makubaliano ya Makka ya Ulinzi wa Pamoja".

Mohammed bin Salman, Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki na Shehbaz Sharif, Waziri Mkuu wa Pakistan walitia saini makubaliano ya ulinzi wa pamoja mjini Makka, ambayo msingi wake mkuu ni kudhamini usalama wa pamoja. Kwa maneno mengine, shambulio la kijeshi dhidi ya taifa lolote kati ya mataifa hayo matatu litachukuliwa kuwa shambulio dhidi ya mataifa yote matatu, ambapo nchi hizo zimeamua kuungana mkono katika kukabiliana na tishio la namna hiyo.

Kuna maswali mengi kuhusu makubaliano hayo, lakini mawili yanaonekana kuwa muhimu zaidi. La kwanza ni kuwa makubaliano hayo yamefikiwa katika mazingira gani? Na la pili, makubaliano hayo ni muhimu kwa kiasi gani?

Kuhusu sababu za kusainiwa makubaliano yenyewe, hoja mbili muhimu zinaweza kuangaziwa.

Hoja ya kwanza ni kwamba usalama wa eneo la Asia Magharibi umepitia mabadiliko makubwa. Utawala wa Kizayuni umeonyesha kivitendo nia yake ya kuvuruga uwiano wa nguvu katika eneo na kujiimarisha kama nguvu kuu inayodhibiti hali ya mambo katika kanda hii. Wakati huo huo, Mhimili wa Muqawama (Axis of Resistance) umeonyesha kuwa hauwezi kuangamizwa, hata kwa mashambulizi ya pamoja ya Marekani na utawala wa Kizayuni, na kwamba unajitahidi kufafanua upya uwezo wake wa kijeshi. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imeonyesha kuwa inamiliki uwezo mkubwa wa kijeshi kwa ajili ya kujilinda, kiasi kwamba hata mashambulizi ya pamoja yaliyofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi yake yaliambulia patupu. Sambamba na matukio haya, imedhihirika wazi kuwa nchi za Kiarabu, ikiwemo Saudi Arabia, ziko katika hali hatari na dhaifu.

Hoja ya pili ni kwamba matukio ya hivi karibuni Asia Magharibi yameonyesha kuwa nchi za eneo haziwezi tena kuendelea kuweka usalama wazo mikononbi mwa nchi za kigeni na hasa Marekani. Kwa upande mmoja, Marekani imeonyesha kuwa utawala wa Kizayuni ndio mshirika wake muhimu zaidi katika eneo, ukipewa kipaumbele kuliko nchi za Kiarabu, huku kwa upande wa pili, mfumo wake wa kushughulikia masuala ya usalama, hasa kuhusiana na vituo vyake vya kijeshi katika nchi za eneo, ukifeli kulinda usalama wa nchi hizo. Isitoshe, mbali na wenyewe kuchochea mashambulizi ya kulipiza kisasi ulishindwa pia kujilinda mbele ya mashambulizi makali ya Iran. Hivyo, kufeli kwa mfumo wa kigeni wa kulinda usalama wa nchi za Kiarabu kunaweza kutajwa kuwa moja ya sababu zilizopelekea kutiwa saini Makubaliano ya Makka.

Swali jingine linajitokeza ni kuwa je, Makubaliano ya Makka yana umuhimu wa kiasi gani?

Umuhimu mkuu wa Makubaliano ya Makka unatokana na jitihada za kuunda upya mfumo wa usalama wa eneo la Asia Magharibi. Kwa upande mmoja, makubaliano haya yanaakisi mwelekeo unaoongezeka miongoni mwa mataifa ya kanda hii wa kutegemea zaidi uwezo wao wa ndani kwa ajili ya kulinda usalama wao, na kwa upande wa pili, yanaonyesha kuwa mfumo wa jadi wa kutegemea kikamilifu mataifa ya nje kwa ajili ya kulinda usalama wa kanda haudhamini hata kidogo maslahi ya wadau wote wanaohusika. Hivyo, kuibuka ushirikiano wa usalama wa pamoja kunaweza kuashiria hamu ya mataifa ya eneo, ya kufafanua upya mfumo wa usalama wa kanda hii.

Pamoja na hayo, ni muhimu kuzingatia kuwa nchi kama vile Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Qatar zimesalia nje ya makubaliano haya, huenda ni kwa sababu hazikualikwa au kwa sababu hazikuwa na nia ya kujiunga. Kwa hivyo, makubaliano ya Makka licha ya kuwa ni muungano wa nchi chache, lakini unawakilisha mataifa matatu muhimu ya Kiislamu, ambayo kabla ya suala jingine lolote, yametoa kipaumbele kwa usalama wa Saudi Arabia. Kabla ya hapo, Saudia tayari ilikuwa imesaini makubaliano ya usalama ya nchi mbili na Pakistan. Mataifa hayo mawili yamekuwa na ushirikiano wa muda mrefu wa kijeshi na kiusalama; hasa, yaliposaini makubaliano ya ulinzi yanayosema kuwa kitendo cha uchokozi dhidi ya taifa moja ni uchokozi dhidi ya taifa la pili. Katika miaka ya karibuni, uhusiano wa ulinzi kati ya Uturuki na Saudi Arabia pia umepanuka, hasa kuhusiana na masuala ya usalama, uhamishaji wa teknolojia, mafunzo na uzalishaji wa pamoja. Hata hivyo, makubaliano hayo hayajafanikiwa kuondoa hofu za kiusalama za Saudi Arabia, na pia hatuwezi kuwa na yakini kwamba makubaliano ya Makka yatapunguza vitisho au kuimarisha usalama wa ufalme huo unaoweka usalama wake mikononi mwa wageni.

Pamoja na hayo, kinachofanya makubaliano ya Makka kuwa na umuhimu ni kwamba ni sehemu ya mwelekeo mpana zaidi ambapo mataifa yenye nguvu katika eneo yanajaribu kuimarisha uwezo wao wa kujidhaminia usalama wao yenyewe bila kuvunja uhusiano na Marekani na nchi nyingine za Magharibi. Mwenendo huu kabla ya kuwa ni kuundwa muungano dhidi ya nchi yoyote mahususi katika eneo, unaakisi jitihada za kupunguza utegemezi wa kiusalama kwa mataifa ya kigeni na kupanua machaguo ya usalama ndani ya eneo.