Iran yapiga kambi na manuwari za Marekani kulipiza kisasi
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) limesema kuwa Kikosi chake cha Anga kimepiga kwa makombora Kituo cha Anga cha al-Azraq cha Marekani huko Jordan na kusisitiza kuwa operesheni hiyo ni ya kulipiza kisasi uchokozi wa Marekani dhidi ya meli za mafuta za Iran.
Katika taarifa iliyotolewa mapema leo Jumatano, Ofisi ya Mahusiano ya Umma ya SEPAH imesema kuwa operesheni hiyo imehusisha "shambulio kubwa la makombora" dhidi ya kituo hicho.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, shambulio hilo kubwa limetumia makombora ya balestiki kupiga maeneo ya matengenezo na maegesho ya ndege za kivita za Marekani za F-35, F-16, na F-15 huko Jordan na kusababisha uharibifu mkubwa.
Kumeenea video nyingi zinazoonyesha shambulio hilo ambazo zinaonesha wimbi la makombora ya Iran yakipiga kituo hicho bila ya kizuizi chochote. Mfumo wa ulinzi wa anga wa Patriot wa Marekani unaonekana kwenye video hizo ukifanya majaribio mengi lakini hayakufanikiwa.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran limesema kuwa, operesheni hiyo ya makombora imefanyika baada ya Marekani kushambulia meli kadhaa za kibiashara na za mafuta za Iran.
"Jeshi la kigaidi la Marekani lililoshindwa kwenye medani ya vita limeamua kushambulia meli za kibiashara na za mafuta za Iran kutokana na kukata tamaa kwenye uwanja wa mapambano," imesema sehemu moja ya taarifa hiyo.
Pia imesema kuwa Muqawama utaendelea kwa nguvu zote na Lango Bahari la Hormuz litaendelea kudhibitiwa na Iran na hakuna chombo chochote kitakachoruhusiwa kupita kwenye lango hilo bila ya idhini ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika taarifa yake nyingine, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH limesema katika tangazo lake nambari 14 kwamba limepiga manuwari za Marekani za DDG-119 na DDG-53 zinazobeba makombora yakiwemo aina ya Aegis.
Sehemu moja ya taarifa ya SEPAH kupitia kitengo chake cha Mahusiano ya Umma inasema: Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu. Piganeni nao, Mwenyezi Mungu awaadhibu kwa mikono yenu, na awahizi (makafiri) na akunusuruni muwashinde na avipoe vifua vya kaumu ya waumini.
Taifa lililoamka la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran;
Katika ujibu vitendo vya ukatili vya jeshi la kigaidi la Shetani Mkuu vya kushambulia meli za mafuta na za biashara za Iran, kikosi chenye nguvu cha anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika operesheni iliyopewa jina la "Yaa Haidar Karrar" ya kumwadhibu mchokozi, limeshambulia manuwari za vita za adui ziitwazo DDG-119 na DDG-53 za kubeba makombora yakiwemo ya Aegis kwa kutumia makombora yenye nguvu ya balistiki. Shambulio hilo la kulipiza kisasi, limeharibu vibaya meli hizo (za kivita za Marekani).