Serikali ya Burundi yakosoa msimamo wa Kenya kuhusu wafanyabiashara wa kigeni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141272-serikali_ya_burundi_yakosoa_msimamo_wa_kenya_kuhusu_wafanyabiashara_wa_kigeni
Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Édouard Bizimana, ameikosoa serikali ya Kenya kwa kusema kuwa maelezo yake kuhusu vibali vya kazi na biashara hayajajibu madai ya vitendo vya ukatili dhidi ya raia wa kigeni, hususan raia wa Burundi.
(last modified 2026-09-07T10:50:45+00:00 )
Sep 07, 2026 10:39 UTC
  • Serikali ya Burundi yakosoa msimamo wa Kenya kuhusu wafanyabiashara wa kigeni
    Serikali ya Burundi yakosoa msimamo wa Kenya kuhusu wafanyabiashara wa kigeni

Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Édouard Bizimana, ameikosoa serikali ya Kenya kwa kusema kuwa maelezo yake kuhusu vibali vya kazi na biashara hayajajibu madai ya vitendo vya ukatili dhidi ya raia wa kigeni, hususan raia wa Burundi.

Katika ujumbe kupitia mtandao wa X, Bizimana amesema Wakenya wanaishi kwa amani nchini Burundi na kuitaka serikali ya Kenya kuhakikisha usalama wa raia wa Burundi wanaoishi nchini humo.

Kauli hiyo imekuja baada ya mkutano wa dharura alioufanya mwishoni mwa wiki na wawakilishi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, akiwemo Kenya.

Bizimana amesema aliombwa kuwasilisha wasiwasi wa Burundi kwa serikali ya Kenya na kuhakikisha raia wa Burundi hawanyanyaswi.

Alipoulizwa kuhusu hatua ambazo serikali ya Burundi inapanga kuchukua, Bizimana amesema ujumbe wake kupitia X ulikuwa wazi na kwamba serikali inafuatilia kwa karibu hali hiyo.

Amesema Burundi haitasita kuchukua hatua iwapo raia wake watadhulumiwa.

Bizimana pia amekosoa wazo la kuwaruhusu raia kufanya majukumu ya polisi, akisema hatua hiyo inaweza kuchochea ghasia, uporaji na chuki dhidi ya wageni.

Serikali ya Kenya imesema wageni wenye vibali halali vya kazi na biashara wanaweza kuendelea na shughuli zao. Hata hivyo, wageni wanaotumia viza za utalii kufanya kazi au biashara wanaweza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Warundi wengi, Waganda, na Watanzania wengi wanafanya kazi nchini Kenya kwenye sekta za uuzaji wa chakula, nguo, na hata ujenzi. Kutokana na mijadala na utata uliojitokeza, mamlaka husika tangu wakati huo zimejaribu kufafanua msimamo wao.

Mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali ya haki za binadamu pia yalilaani matamshi ya Rais William Ruto, yakibainisha kwamba tangazo lake lilikuwa hatarini "kuchochea ubaguzi na chuki dhidi ya wageni."