Mume wa Rais Samia Suluhu Hassan aaga dunia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141270-mume_wa_rais_samia_suluhu_hassan_aaga_dunia
Mume wa Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw.Hafidh Ameir Hassan ameaga dunia hii leo tarehe 07 Septemba, 2026.
(last modified 2026-09-07T10:32:22+00:00 )
Sep 07, 2026 10:29 UTC
  • Hafidh Ameir
    Hafidh Ameir

Mume wa Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw.Hafidh Ameir Hassan ameaga dunia hii leo tarehe 07 Septemba, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hii leo na Makamu wa Rais wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, Bw. Hafidh alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya kumbukumbu ya Emilio Mzena visiwani Zanzibar.

"Ndugu wananchi, kwa masikitiko makubwa, nawajulisha taarifa ya kifo cha Muheshimiwa Hafidh Ameir Hassan, mume wa rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, muheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kilichotokea leo 07. Septemba 2026 majira ya saa mbili asubuhi katika hospitali ya kumbukumbu ya Emilio Mzena Zanzibar, alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo. Ninatoa pole kwa muheshimiwa rais, familia, ndugu jamaa na marafiki na watanzania wote kwa msiba," alisema Makamu wa rais Ndejembi.

Mipango ya mazishi inaendelea kufanyika Kizimkazi Zanzibar.

Rais wa Kenya William Ruto ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kufuatia kifo cha mumewe, Hafidh Ameir Hassan.

Katika ujumbe wake, Rais Ruto amesema amepokea kwa huzuni kubwa taarifa za kifo cha Hafidh, akitoa pole kwa Rais Samia, familia yake na Watanzania wote.

Amesema kifo hicho kimemnyang'anya Rais Samia mwenza wake wa maisha, watoto wake baba yao mpendwa, na Tanzania imepoteza mwananchi wake mashuhuri.

“Kenya iko pamoja na ndugu na dada zetu wa Tanzania katika kipindi hiki cha majonzi,” amesema Rais Ruto.

Ameomba Mungu awape Rais Samia na familia yake faraja na nguvu katika kipindi hiki kigumu, na amuimarishe Hafidh Ameir Hassan katika pumziko la milele.