Iran yazindua programu mpya ya kinga-virusi iliyotengenezwa nchini
Sambamba na maonyesho ya kimataifa ya Iran ya ELECOMP 2026, ambayo ni maonyesho makubwa zaidi ya nchi kwa sekta za elektroniki, teknolojia za kompyuta, na biashara pepe (e-commerce), Iran imezindua programu yake ya pili ya kinga-virusi (antivirus) iliyotengenezwa nchini, ijulikanayo kama Ayyza. Programu hii hutumia akili mnemba (AI) na mbinu za kujifunza kwa mashine (machine learning) kutambua virusi vipya visivyojulikana na vitisho vya mtandaoni ambavyo havijatambulika awali.
Kundi la maofisa wakuu kutoka sekta za usalama, ulinzi, mtandao wa kompyuta, na kampuni zinazojishughulisha na teknolojia za ndani (knowledge-based firms) walihudhuria sherehe za uzinduzi wa programu hiyo mpya ya taifa ya kinga-virusi. Hafla hiyo ilifanyika pembezoni mwa toleo la 29 la Maonyesho ya ELECOMP, yaliyofanyika kuanzia Agosti 31 hadi Septemba 3, mjini Tehran.
Ayyza inajumuisha teknolojia za XDR (Extended Detection and Response), EDR (Endpoint Detection and Response), na kinga-virusi (antivirus) katika mfumo mmoja wa kiusalama. Imeundwa kutoa suluhisho la kitaifa na la kitaalamu dhidi ya vitisho vinavyolenga miundombinu na mali za kidijitali za nchi.
Programu hii ni ushahidi mwingine wa kuongezeka kwa utaalamu wa kisayansi wa Iran na hatua zake za kimkakati katika kujenga ustahimilivu wa mtandao na kujitegemea kwa taifa, katika wakati ambapo shughuli za kiuchumi, benki, viwanda, mawasiliano na huduma zinazotegemea mifumo ya kidijitali zinahitaji ulinzi wa miundombinu ya mtandao zaidi ya zamani wowote.
Kinga-virusi (antivirus), kama mojawapo ya tabaka za msingi za ulinzi wa mtandao, inasimama mstari wa mbele katika kutambua na kupambana na programu hasidi (malware). Ayyza ni sehemu ya mkakati wa Iran katika nyanja ya ulinzi wa kujilinda, zinazosisitiza kuegemea uwezo wa ndani, kukuza bidhaa asilia, na kupunguza utegemezi kwa teknolojia za kigeni.
Programu ya Ayyza ni zao la uwekezaji katika maarifa, rasilimali watu maalumu, na uwezo wa uhandisi wa ndani. Uzinduzi wake unaweza kuonekana kama ishara ya sekta ya usalama wa mtandao ya Iran kuhama kutoka kuwa mtumizi hadi kuwa mbunifu wa bidhaa za kimkakati.
Maonyesho ya ELECOMP 2026 yalifanyika kwa uwepo wa washiriki zaidi ya 350 katika kumbi 14 za maonyesho, yakijumuisha maeneo kama akili mnemba (AI), usalama wa mtandao, programu na maunzi ngumu na maunzi laini (software na hardware), huduma za kidijitali, na biashara za kibunifu.