Namna vita na vikwazo vinavyounganisha uchumi wa Iran na Russia
-
Vita na vikwazo vinavyounganisha uchumi wa Iran na Russia
Hamjambo wapendwa wasikilizaji na karibuni kuwa nasi tena katika kipindi cha Makala ya Wiki. Kipindi chetu kinaangazia vikwazo vya Marekani na washirika wake dhidi ya Iran na jinsi viilivyochangia kuunganisha uchumi wa Jamhuri ya Kiislamu na Russia. ******
Mwezi uliopita, Ukraine ilishambulia meli ya mizigo ya Iran katika Bahari ya Kaspi (Caspian) na kusababisha kifo cha baharia mmoja; ambapo Kiev ilidai kuwa shambulio hilo lililenga meli zinazohusika na usafirishaji wa mizigo ya kijeshi. Tehran ilisisitiza kuwa meli hiyo ilikuwa ya kibiashara na kutangaza kuwa italipiza kisasi.
Tukio hilo, ambalo lilidhibitiwa kupitia mashauriano ya kidiplomasia yaliyolenga kupunguza mivutano, lilizua hofu kuhusu mfungamano unaozidi kuongezeka kati ya vita vya Ukraine na vile vya Asia Magharibi.
Tukio hilo pia ilifichua nyanja mpya ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Iran na Russia, ushirikiano unaovuka mipaka ya biashara ya kawaida na kuingia katika mfumo mpana zaidi wa ushirikiano wa kiviwanda na uwekezaji.
Maafisa wakuu kutoka nchi zote mbili, walisisitiza pambizoni mwa mikutano ya kundi la BRICS na Tume ya Pamoja ya Uchumi kuhusu udharura wa kuandaa ramani ya pamoja ili kusonga mbele zaidi kuelekea upande wa kuwa na muungano mkubwa ili kujitegemea baina yao.
Shinikizo la kijiografia linalozikwamisha nchi mbili za Iran na Russia kufikia masoko, mitaji na fedha za kimataifa kwa wakati mmoja limepelekea kuwepo umuhimu kwa nchi hizo kuimarisha pakubwa ushirikiano wa kibiashara, kifedha na kiviwanda baina ya pande mbili.
Katika muktadha huu, ramani ya pamoja ya utekelezaji inawakilisha hatua mpya kutoka kwenye ushirikiano unaozingatia miradi kuelekea uundaji wa minyororo ya pamoja ya thamani na uwekezaji.
Bahari ya Kaspi ambayo ndiyo eneo kubwa zaidi la maji duniani lililo ndani ya dola (nchi) imekuwa mojawapo ya njia muhimu zaidi za biashara kati ya Iran na Russia; jambo linalosisitiza umuhimu wake wa kimkakati unaozidi kukua kama njia ya usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
Bandari nne za Iran kwenye pwani ya Bahari ya Kaspi au Caspian zinafanya kazi usiku na mchana kupakua mizigo na aina mbalimbali za bidhaa kama ngano, mahindi, na mafuta ya alizeti.
Katika miezi minne ya kwanza ya mwaka huu wa 2026 usafirishaji wa mizigo katika ukanda wa Kaskazini-Kusini uliongezeka kwa asilimia 87 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita. Russia pia imeshuhudia ongezeko la zaidi ya asilimia 56 katika mauzo yake ya bidhaa mbalimbali kwenda Iran kupitia njia hiyo.
Ukuaji huu wa biashara unaashiria kuwa njia za kaskazini, hasa ukanda wa Kaskazini-Kusini, ni mojawapo ya njia kuu za biashara kati ya Iran na Russia.
Uwezo wa kushughulikia kazi za forodha katika njia ya magharibi ya ukanda huo inayopitia Azerbaijan pia umeongezeka mara tano na kufikia malori 1,900 kwa siku.
Ukanda wa Kimataifa wa Usafirishaji wa Kaskazini-Kusini ndio mradi muhimu zaidi wa miundombinu kwa nchi za Iran na Russia, na ni uti wa mgongo wa ramani ya pamoja ya utekelezaji.
Mtandao huu wa usafirishaji unaunganisha St. Petersburg na bandari ya Mumbai, na unajumuisha njia kuu tatu: Njia ya kuvuka Bahari ya Kaspi, njia ya magharibi, na njia ya mashariki.
Mradi wa reli ya Rasht-Astara ni kiungo kinachokosekana katika njia ya magharibi ya ukanda huo. Maafisa kutoka nchi zote mbili wamesisitiza udharura wa utekelezaji wa mradi huo, na inatarajiwa kuwa ujenzi wake utaanza pindi hali ya eneo hilo itakapotulia.
Kukamilika kwa mradi huu kutafanya njia ya Russia kufika kwenye masoko ya kusini na maji ya Bahari ya Hindi kuwa fupi na yenye machaguo mengi zaidi, huku ukiimarisha nafasi ya Iran kama kitovu cha usafirishaji na usafiri wa kimataifa katika eneo hilo. ******
Mojawapo ya mafanikio yanayoonekana ya ushirikiano kati ya Iran na Russia ni ustawi na maendeleo katika sekta ya fedha na benki. Mifumo ya malipo ya Shetab ya Iran na Mir ya Russia imeunganishwa rasmi, na muunganiko huo unatekelezwa katika awamu tatu.
Katika awamu ya kwanza, watumiaji wa Iran wanaweza kutoa fedha sarafu ya riali kutoka kwenye mashine za kutolea fedha (ATM) nchini Russia, huku awamu zinazofuata zikilenga kuwezesha matumizi ya kadi za Russia nchini Iran na malipo katika maduka ya rejareja.
Zaidi ya asilimia 80 ya biashara ya nchi mbili sasa zinafanyika kwa kutumia sarafu za kitaifa, na upanuzi wa uhusiano wa kibenki wa uwakilishi kati ya benki za biashara za pande mbili ni suala lililopo kwenye ajenda.
Kuanzishwa kwenye mfumo wa forodha wa kidijitali uliounganishwa na utekelezaji wa utaratibu wa ukanda wa kijani kibichi kwa ajili ya kupata idhini rasmi ni miongoni mwa mipango mingine iliyokubaliwa ambayo inaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa muda wa kushughulikia taratibu za forodha.
Katika sekta ya nishati; ushirikiano kati ya nchi hizo mbili unaendelea katika nyanja mbalimbali. Kampuni za Russia zimewekeza katika maeneo saba ya visima vya mafuta nchini Iran. Hii ni katika hali ambayo ujenzi wa awamu za pili na tatu za kituo cha nishati ya nyuklia cha Bushehr unaendelea huku vifaa vinavyohitajika vikitengenezwa nchini Russia.
Mnamo mwezi Juni mwaka huu Iran na Russia zilitangaza kusainiwa mkataba wa maelewano wenye thamani ya dola bilioni 25 kwa ajili ya ushirikiano katika miradi ya nyuklia. Mradi wa Hormuz, ambao ndio mpango mkubwa zaidi wa nyuklia wa Iran unaendelezwa kwa ushirikiano na sekta binafsi na kampuni ya serikali ya Rosatom.
Mazungumzo pia yanaendelea kuhusu makubaliano ya kina ya kupitisha gesi kutoka Russia na ushirikiano katika mitambo midogo ya nyuklia.
Ikiwa Bahari ya Kaspi ndiyo njia ya muunganiko huu, Ukanda wa Kaskazini-Kusini ndiyo miundombinu yake, na mifumo ya kifedha ndiyo nyenzo zake- basi ushirikiano wa kiviwanda ndilo lengo la mwisho.
Naibu Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Iran amesisitiza umuhimu wa kuvuka mipaka ya biashara ya kawaida na kuelekea kwenye ushirikiano endelevu, uwekezaji wa pamoja na uundaji wa minyororo ya thamani ya viwanda na biashara.
Uzalishaji wa pamoja wa nyenzo za viwandani, vifaa vya mitambo ya kuzalisha umeme, mashine nzito na magari ni miongoni mwa nguzo kuu za ushirikiano huo. Biashara ya nchi mbili ilifikia takriban dola bilioni 5.8 mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 21 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake.
Utekelezaji kamili wa makubaliano ya biashara huria kati ya Iran na Muungano wa Kiuchumi wa Eurasia ulioanza Mei 2025, umeweka msingi wa ukuaji wa asilimia 15 katika biashara ya Iran na nchi wanachama katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji wake.
Hata hivyo, kufikia lengo la dola bilioni 20 kunategemea mambo yanayovuka mipaka ya ufafanuzi wa miradi ya pamoja, ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa mifumo ya kisheria na taratibu za kudhibiti hatari kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda.
Uzalishaji wa pamoja wa mitambo mizito unahitaji uwekezaji mkubwa wa muda mrefu. Ili kuimarisha ushirikiano, nchi mbili Iran na Russia zitahitaji kwenda mbali zaidi ya kufadhili miradi na kuwekeza moja kwa moja katika makampuni ya uzalishaji na teknolojia.
Mkataba wa Ushirikiano wa Kimkakati wa Kina uliotiwa saini mwezi Januari 2025 umeimarisha mfumo wa kisheria wa ushirikiano huo.
Mashinikizo yanayotokana na vikwazo na vizuizi vya kufikia masoko ya fedha na biashara ya nchi za Magharibi pia yamezidisha hamu ya nchi mbili kuanzisha mifumo huru ya malipo, usafirishaji na uwekezaji.
Wakati huo huo mawasiliano yanayoendelea kati ya taasisi za ulinzi na kidiplomasia yanaonyesha kiwango cha juu cha uratibu wa kimkakati. Hata hivyo, kubadilisha mfumo huo wa kimkakati kuwa biashara na uwekezaji wa kiwango cha juu bado kunakabiliwa na changamoto.
Katika baadhi ya masoko ya nishat, maslahi ya Iran na Russia yanahusisha ushirikiano na ushindani. Hata hivyo, uwezekano wa ushirikiano katika nyanja za viwanda, nishati na usafirishaji unaonyesha kuwa wigo wa ushirikiano ni mpana zaidi kuliko hali ya sasa.
Vita na vikwazo vimezidisha ulazima wa ushirikiano wa karibu zaidi kati ya Iran na Russia- lakini umuhimu wa ushirikiano huo haukomei kwenye namna nchi hizo mbili zinavyokabiliana na mashinikizo ya nje.
Ramani ya pamoja ya utekelezaji inatoa fursa ya kuvuka hatua ya kuongeza tu kiasi cha biashara na kuelekea katika kujenga minyororo ya thamani, uwekezaji wa pamoja na uhusiano wa muda mrefu wa kiviwanda.
Ukanda wa Kaskazini-Kusini, ukiwa na ukuaji wa ajabu wa asilimia 87 katika miezi minne ya kwanza ya mwaka 2026 na ongezeko la asilimia 56 la mauzo ya bidhaa za Russia kwenda Iran, umeonyesha kuwa mfumo wa ushirikiano unakuwa uhalisia unaoonekana.
Iwapo kasi hii itaendelea, uhusiano wa kiuchumi kati ya Tehran na Moscow unaweza kubadilika kutoka ushirikiano unaochochewa na mahitaji ya muda mfupi na kuwa nguzo imara ya ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda, jambo litakalofungua fursa mpya kwa nchi zote mbili katika dunia inayozidi kuwa na vituo vingi vya nguvu. *****
Muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi chetu umemalizika. Tukutane tena katika kipindi kijacho panapo majaaliwa ya Mola Muumba.