Afrika Kusini yatoa mwito kwa BRICS kutetea ushirikiano wa pande nyingi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141438-afrika_kusini_yatoa_mwito_kwa_brics_kutetea_ushirikiano_wa_pande_nyingi
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ametoa mwito kwa nchi za BRICS kuimarisha ushirikiano wa pande nyingi na kushinikiza mageuzi ya mfumo wa kimataifa akisema kuwa sauti za Afrika na nchi za kusini mwa dunia lazima zisikike kikamilifu kimataifa.
(last modified 2026-09-14T07:34:59+00:00 )
Sep 14, 2026 07:32 UTC
  • Afrika Kusini yatoa mwito kwa BRICS kutetea ushirikiano wa pande nyingi

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ametoa mwito kwa nchi za BRICS kuimarisha ushirikiano wa pande nyingi na kushinikiza mageuzi ya mfumo wa kimataifa akisema kuwa sauti za Afrika na nchi za kusini mwa dunia lazima zisikike kikamilifu kimataifa.

Ikulu ya Afrika Kusini imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, Rais Ramaphosa amesema hayo katika Mkutano wa 18 wa BRICS huko New Delhi, India.

Amesema, itibari na mamlaka ya Umoja wa Mataifa (UN) na misingi ya ushirikiano wa pande nyingi iko hatarini hivi sasa kwani taasisi na sheria za kimataifa "zinapuuzwa na kupotoshwa" na baadhi ya madola duniani.

Ramaphosa ameongeza kuwa, Afrika Kusini inapigania kuweko mfumo wa kimataifa unaotabirika na unaoheshimu sheria za kimataifa. Mfumo ambao utaheshimu vipengee vya Hati ya Umoja wa Mataifa. Amesema: Amri iliyoanzishwa juu ya usawa wa nchi huru, uadilifu wa eneo na uhuru wa kisiasa inapaswa kuyafaidisha mataifa yote, makubwa na madogo.

"BRICS inapaswa kubaki kuwa sauti ya pamoja ya mageuzi, kuonesha matunda mazuri ya ushirikiano wa pande nyingi na kusaidia kuunda mfumo wa utawala wa kimataifa wenye haki, uwajibikaji zaidi na unaozingatia maendeleo," amesema.

Vile vile amesema: "Lazima tuimarishe ushirikiano wa pande nyingi kupitia mageuzi na kivitendo. Na lazima tuhakikishe kwamba sauti za Afrika na ya nchi za kusini mwa dunia zinaakisiwa na kuheshimiwa kikamilifu katika kuunda mfumo bora wa kimataifa wa siku zijazo."

Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Dkt. Masoud Pezeshkian, ametoa wito kwa kundi la mataifa yanayoinukia kiuchumi la BRICS kuchukua jukumu “lenye ufanisi zaidi” katika kulinda mamlaka ya kitaifa na kusimamia kanuni ya kimataifa ya kutotumia nguvu, hasa katika kipindi hiki cha sasa chenye changamoto nyingi.

Rais Pezeshkian alisema hayo jana Jumapili katika hotuba yake kwenye Mkutano huo wa 18 wa Viongozi wa BRICS, unaofanyika katika mji mkuu wa India, New Delhi, chini ya kaulimbiu: “Kujenga kwa Ajili ya Ustahimilivu, Ubunifu, Ushirikiano na Uendelevu.”