Putin: Watu wa Iran wanapigania kwa ushujaa uhuru wao wa kitaifa
-
Rais Vladimir Putin wa Russia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi
Rais wa Russia, Vladimir Putin, amesema kuwa wananchi wa Iran wanapigana kwa ujasiri na kishujaa kulinda mamlaka yao ya kitaifa. Putin ameyasema hayo mjini Moscow katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi.
Putin alikutana na waziri huyo mjini St. Petersburg, ambapo aliwapongeza wananchi wa Iran kwa “kupigania uhuru wao kwa ujasiri na kishujaa”, akieleza matumaini kuwa wataweza kuvuka kipindi hiki kigumu na kwamba amani itarejea nchini humo.
Amesisitiza kuwa Russia itachukua hatua zote muhimu kulinda maslahi ya Iran na nchi nyingine za eneo hilo, pamoja na kusaidia kurejesha amani haraka iwezekanavyo.
Rais Vladimir Putin ameongeza kwamba Russia itachukua kila hatua inayohitajika ili kulinda maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na nchi nyingine za kieneo, na pia kusaidia kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo kwa haraka iwezekanavyo.
Rais wa Russia ameeleza kuwa wiki iliyopita alipokea ujumbe wa maandishi kutoka kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei.
Aidha, alitoa tena salamu za rambirambi kwa kufuatia kuuawa kishahidi Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, makamanda waandamizi wa kijeshi, maafisa wa serikali ya Iran pamoja na raia, katika mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Putin amesisitiza kuwa Russia imeazimia kuimarisha ushirikiano wa kimkakati wa muda mrefu kati ya Tehran na Moscow.
Kwa upande wake, Araghchi, aliyekuwa katika hatua ya mwisho ya ziara yake ya kikanda, ameipongeza Russia kwa kuendelea kuiunga mkono Iran, hususan katika vita vya uchokozi vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa Israel.
Amesema: “Mahusiano kati ya Russia na Iran, ambayo ni ya kimkakati, yataendelea kuimarika,” akiongeza kuwa wananchi wa Iran, kwa ujasiri wao, wamefanikiwa kupinga mashinikizo ya Marekani na wataweza kustahimili hali hiyo.
Waziri huyo pia amewasilisha salamu za dhati za Kiongozi wa Mapinduzi kwa rais wa Russia.
Araghchi aliwasili mjini Moscow Jumapili usiku katika hatua ya mwisho ya ziara yake iliyompeleka pia katika nchi za Pakistan na Oman.
Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Russia amesema Iran na Russia zitasimama bega kwa bega katika mazingira yaliyojitokeza kutokana na hatua za uchokozi zisizo za kisheria za Marekani zinazoilenga Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Andrey Belousov alitoa matamshi hayo Jumatatu wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Ulinzi wa Iran, Reza Talaei-Nik, katika mji mkuu wa Kyrgyzstan, Bishkek.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tass, Belousov amesema kuwa msaada huo utaendelea “kama ilivyokuwa awali, bila kujali namna hali itakavyoendelea kubadilika.”