Mashambulizi mapya ya Yemen yaangamiza mamluki wa Saudia wasiopungua 58
-
Mamluki wa Saudia wasiopungua 58 wauawa Yemen
Vikosi vya ulinzi vya Yemen vimefanya operesheni kubwa iliyozilenga ngome za kijeshi na vituo vikuu vya kamanda za kijeshi zilizokuwa zikisimamiwa na mamluki wanaoungwa mkono na Saudi Arabia nchini humo.
Vyombo vya habari vya Yemen jana Alhamisi vilitangaza kuwa kuwa operesheni hiyo ilihusisha uvurumishwaji wa makombora mengi ya balistiki na ndege zisizo na rubani (droni) dhidi ya adui na vituo vyao vya kamandi za kijeshi katika eneo la al-Ruwaik mkoani Ma’rib, na katika wilaya za al-Abr, al-Thaniyah na al-Wadiah katika Mkoa wa Hadhramaut.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha al-Masirah, chanzo cha kuaminika katika jeshi la Yemen kuliarifu kuwa operesheni hiyo iliua na kujeruhi mamluki wengi wanaoshirikiana na Saudi Arabia, huku ikiharibu kambi zao za kijeshi, ghala za silaha na magari ya kivita.
Mashambulizi mapya ya Yemen yameua mamluki wa Saudia wasiopungua 58 na kujeruhi makumi ya wengine, kimebainisha chanzo cha kijeshi cha Saudi Arabia kilipozungumza na shirika la habarti la AFP kwa sharti la kutotajwa jina.
Wakati huo huo, Gavana wa mkoa wa Ma’rib, Ali Tuaiman, na Gavana wa Hadhramaut, Luqman Baras, wamewatahadharisha wananchi wa Yemen kuhusu kupigana upande wa adui.
Inafaa kuashiria hapa kuwa Saudi Arabia ilianzisha vita vya uharibifu dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015, lakini ilishindwa kuurejesha mamlakani nchini humo utawala unaoiunga mkono Riyadh.