Baghaei ajibu madai ya Saudi Arabia kuhusu kushambuliwa mji mtakatifu wa Makka
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141536-baghaei_ajibu_madai_ya_saudi_arabia_kuhusu_kushambuliwa_mji_mtakatifu_wa_makka
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, madai ya kuzuia ndege isiyo na rubani iliyokuwa ikielekea katika mji mtakatifu wa Makka hayawezi kuwa msingi wa kuutuhumu upande wowote.
(last modified 2026-09-18T03:54:26+00:00 )
Sep 18, 2026 03:52 UTC
  • Esmail Baghaei, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran
    Esmail Baghaei, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, madai ya kuzuia ndege isiyo na rubani iliyokuwa ikielekea katika mji mtakatifu wa Makka hayawezi kuwa msingi wa kuutuhumu upande wowote.

Esmail Baghaei, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, amesema hayo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X kuhusu madai ya kuzuia ndege hiyo isiyo na rubani iliyokuwa ikielekea Makka Tukufu na kueleza kwamba,

Kitendo chochote cha kuvamia au kulenga maeneo matakatifu ya Kiislamu, hususan Makka al-Mukarramah, Madinat al-Munawwarah na Msikiti wa Al-Aqsa, pamoja na kutishia mahujaji na wakazi wa maeneo hayo, kinapaswa kulaaniwa.”

Ameongeza:

Hata hivyo, madai pekee kwamba ndege isiyo na rubani imezuiwa ikiwa njiani kuelekea Makka Tukufu hayawezi kuwa msingi wa kuutuhumu upande fulani; hasa ikizingatiwa kwamba Serikali ya Mabadiliko na Ujenzi ya Yemen imekanusha wazi madai hayo.”

Baghaei amesisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza umuhimu wa kuzuia suala la maeneo matakatifu ya Kiislamu kuingizwa katika siasa na masuala ya kiusalama, pamoja na kutumiwa kama chombo cha kuchochea fitina na kuongeza mvutano katika eneo hilo.

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje pia ameandika:

Haipaswi kusahaulika kwamba eneo letu limekumbwa na matukio kadhaa ya operesheni za ‘bendera ya uongo’, hususan katika miezi ya hivi karibuni. Lengo la operesheni hizo limekuwa kugeuza fikra za umma kutoka kwenye jinai zilizotekelezwa na utawala wa Kizayuni na Marekani katika eneo hili na kuchochea mgawanyiko miongoni mwa nchi za Kiislamu.”

Wakati huo huo, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya wananchi wa Yemen, Ansarullah, imesisitiza tena msimamo wa serikali ya Sana'a wa kukanusha vikali madai ya Saudi Arabia kwamba Jeshi la Yemen linatishia kuyashambulia maeneo matakatifu katika mji wa Makka nchini Saudia.