Wabunge wa Uganda watilia shaka uamuzi wa serikali kutaka kupeleka wanajeshi Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140484-wabunge_wa_uganda_watilia_shaka_uamuzi_wa_serikali_kutaka_kupeleka_wanajeshi_ghaza
Baadhi ya wabunge wa upinzani nchini Uganda wametilia shaka uamuzi wa serikali wa kutaka kupeleka wanajeshi wa nchi hiyo huko Ukanda wa Ghaza watakaokuwa sehemu ya kikosi cha kimataifa cha kurejesha uthabiti katika eneo hilo la ardhi ya Palestina.
(last modified 2026-08-07T12:28:44+00:00 )
Aug 07, 2026 12:27 UTC
  • Wabunge wa Uganda watilia shaka uamuzi wa serikali kutaka kupeleka wanajeshi Ghaza

Baadhi ya wabunge wa upinzani nchini Uganda wametilia shaka uamuzi wa serikali wa kutaka kupeleka wanajeshi wa nchi hiyo huko Ukanda wa Ghaza watakaokuwa sehemu ya kikosi cha kimataifa cha kurejesha uthabiti katika eneo hilo la ardhi ya Palestina.

Mbunge Hassan Kirumira amesema, hatua hiyo ya serikali ya Kampala inaweza kuzua “hofu za kidiplomasia” kwa kuwa Uganda ni mwanachama wa Jumuiya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).

Akizungumza katika kikao cha bunge, Kirumira ameuliza suali kwa waungaji mkono wa uamuzi huo akisema: “Jeshi letu litakuwa linapigana upande gani?”

Hayo yanajiri baada ya bunge la Uganda kuidhinisha ombi la serikali la kutuma wanajeshi wa nchi hiyo huko Ghaza kama sehemu ya Kikosi cha Kimataifa cha Kuleta Uthabiti kilichopendekezwa na iitwayo Bodi ya Amani iliyoundwa na Rais wa Marekani Donald Trump, kwa lengo la kuhakikisha usalama unarejea katika eneo hilo baada ya vita vya kinyama vilivyoanzishwa na utawala wa kizayuni wa Israel.

Hoja hiyo, iliyowasilishwa na Waziri wa Ulinzi Kiryowa Kiwanuka, imepitishwa na Bunge na kuwa ishara ya kwanza ya wazi kwamba Uganda iko tayari kushiriki katika Kikosi cha Kimataifa cha Kuleta Uthabiti huko Ghaza. Morocco ni nchi nyingine ya Kiafrika ambayo tayari imeahidi kuchangia wanajeshi wake kwa ajili ya operesheni hiyo.

Hadi sasa hakuna ufafanuzi wowote uliotolewa ni kwa nini Uganda imekubali kupeleka wanajeshi katika eneo hilo la Palestina.

Waziri wa Ulinzi, Kiryowa Kiwanuka, akiomba uungwaji mkono wa wabunge alisema, Uganda ina uwezo wa kijeshi uliotokana na uzoefu wake katika misheni za kulinda amani katika nchi mbalimbali, ikiwemo Somalia.

Kikosi hicho cha kurejesha uthabiti Ghaza kilipendekezwa na Bodi ya Amani ya Trump mwezi Februari, na kinatarajiwa kuongozwa na Meja Jenerali wa Marekani Jasper Jeffers. Jeffers alisema mwezi Mei kwamba kikosi hicho kitakachokuwa na wanajeshi wapatao 20,000 kitasaidia kuhakikisha “ustawi wa baadaye na amani ya kudumu”…/