Spika Qalibaf: Mkakati wa Marekani wa vitisho na kuvunja ahadi umefeli
-
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Bagher Qalibaf
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Bagher Qalibaf, amekosoa miamala ya hivi karibuni ya Washington kama “diplomasia ya maigizo” isiyo na mashiko, akitangaza kuwa mkakati wa Marekani wa vitisho, kuvunja ahadi, na kusuka simulizi za uongo umefeli. Aidha amesisitiza kwamba Iran haitashiriki katika michezo hiyo ya kuigiza tena.
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X, jioni ya Alhamisi, Qalibaf alionyesha jinsi hali ilivyobadilika haraka kutoka vitisho vya “shambulio kubwa” hadi miito ya ghafla ya mazungumzo, akielezea hilo kama mzunguko wa mara kwa mara wa diplomasia ya kitanzi.
Qalibaf amesisitiza kuwa kutegemea ubabe, ahadi zisizotekelezwa, na habari za uongo kama mbinu ya shinikizo ni mkakati ulioshindwa. Ametoa wito kwa upande wa pili kutambua uhalisia wa mambo na kuheshimu ahadi za awali za usitishaji vita badala ya kuendeleza mzunguko wa vitisho tupu na mabadiliko ya ghafla ya msimamo.
Matamshi haya yanakuja wakati maafisa wa Iran wakizidi kusisitiza msimamo wa kimsingi wa Jamhuri ya Kiislamu mbele ya shinikizo za nje, wakisisitiza kuwa diplomasia ya kweli inahitaji uaminifu na kufuata makubaliano ya awali badala ya maonyesho ya nguvu feki yanayofuatwa na kurudi nyuma kwa haraka.
Tawala zitendazo jinai za Marekani Israel kwa pamoja zilianzisha vita vya kichokozi dhidi ya Iran mnamo Februari 28 kwa kulenga maafisa wa ngazi ya juu wa Iran na pia shule ya msingi huko Minab, kusini mwa nchi hiyo, na kusababisha mauaji ya watoto 168, walimu, na wazazi.
Kama jibu, vikosi vya ulinzi vya Iran vilianzisha mashambulizi makali ya kulipiza kisasi dhidi ya ngome za kijeshi na kiuchumi za Marekani na Israel katika eneo, na kusababisha pigo nzito kwa muungano huo wa shari. Vita hivyo vilisitishwa baada ya siku 40 kwa usitishaji vita, ambao baadaye uliidhinishwa rasmi katikati ya Juni kwa kusainiwa kwa Mkataba wa Maelewano wa Islamabad na marais wa Iran na Marekani.
Hata hivyo, siku chache tu baada ya kusaini hati hiyo, Marekani ilianza kukiuka masharti ya maelewano hayo, na kuwasha tena mzunguko mwingine wa vita ambapo Marekani ililenga miundombinu ya kiraia katika majimbo ya kusini mwa Iran. Iran ilijibu kwa mashambulizi ya usahihi wa hali ya juu, ikitumia makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya kambi za Marekani kote Asia Magharibi, zikiwemo Bahrain, Kuwait, na Jordan.
Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa ametishia kuanzisha shambulio kubwa dhidi ya Iran wiki iliyopita, ikiwemo kulenga miundombinu ya nishati ya nchi hii; hata hivyo, baadaye alirudi nyuma, kutokana onyo la Iran kuwa italipiza kisasi vikali. Aidha duru zinasema ukosefu wa akiba muhimu ya kukabiliana na mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran ni sababu nyingine ambayo imepelekea Marekani isitishe uchokozi wake wakati huu.