Pezeshkian: Iran itaunga mkono maamuzi yatakayochukuliwa na viongozi wa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140450-pezeshkian_iran_itaunga_mkono_maamuzi_yatakayochukuliwa_na_viongozi_wa_palestina
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu itaunga mkono mpango au uamuzi wowote utakaopitishwa na viongozi wa Palestina katika mchakato wa mazungumzo yanayoendelea, akithibitisha tena uungaji mkono thabiti wa Tehran kwa mapambano ya Palestina.
(last modified 2026-08-06T03:55:06+00:00 )
Aug 06, 2026 03:53 UTC
  • Rais Masoud Pezeshkian
    Rais Masoud Pezeshkian

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu itaunga mkono mpango au uamuzi wowote utakaopitishwa na viongozi wa Palestina katika mchakato wa mazungumzo yanayoendelea, akithibitisha tena uungaji mkono thabiti wa Tehran kwa mapambano ya Palestina.

Katika mazungumzo ya simu na Khalil al-Hayya, mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, Rais Pezeshkian amempongeza kwa wadhifa wake mpya na kuelezea matumaini kuwa uongozi wake utakuwa na manufaa kwa wananchi wa Palestina na wakazi wa Ukanda wa Gaza. Rais wa Iran ametoa heshima kwa mashahidi wa Palestina, hususan kiongozi wa kisiasa wa Hamas, marehemu Ismail Haniyeh, ambaye kumbukumbu ya kuuawa kwake inaadhimishwa. Amekitaja kuuawa shahidi Haniyeh wakati wa ziara yake nchini Iran kuwa ni “kitendo cha kihalifu na cha dhulma” kilichofanywa na utawala wa Kizayuni. Ikumbukwe kuwa Haniyeh aliuawa na utawala huo wa Kizayuni mnamo Julai 31, 2024, akiwa safarini mjini Tehran kuhudhuria sherehe za kuapishwa Rais Pezeshkian.

Akisifu ushujaa na uwezo wa kustahamili wa wananchi wa Palestina mbele ya mashambulizi ya Kizayuni, Rais Pezeshkian amesema kuwa nyoyo za wananchi na viongozi wa Iran “zitabaki daima pamoja na wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina,” akiongeza kuwa Iran itaendelea kuunga mkono na kulihami taifa la Palestina “kwa kadiri ya uwezo wake wote.” Rais pia amepongeza juhudi za al-Hayya katika kuimarisha uratibu miongoni mwa makundi ya Palestina.

Mazungumzo hayo yanakuja wakati ambapo Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kile alichokiita makubaliano ya “kihistoria” ambayo kwayo Hamas na makundi mengine ya mapambano ya ukombozi wa Palestina yanapaswa kukabidhi silaha zao. Hamas imepinga maelezo hayo, ikisisitiza kuwa haitakubali kuweka silaha chini ila baada ya utawala wa Kizayuni kutimiza wajibu wake chini ya makubaliano hayo. Makundi mengine ya muqawama ya Palestina pia yamekataa tafsiri ya Washington, yakisisitiza kuwa kuweka chini silaha kunaweza kufanyika tu baada ya kuanzishwa taifa huru la Palestina.

Rais Pezeshkian amesema kuwa kadhia ya Palestina inaendelea kuwa katika nafasi kuu kwenye sera za kigeni za Iran licha ya matukio ya sasa ya kikanda, akiitaja kuwa “kadhia ya kwanza ya Umma wa Kiislamu.” Pia ametoa wito wa kuwepo umoja na mshikamano zaidi miongoni mwa mataifa ya Waislamu, akisema kuwa ushirikiano wa karibu unaweza kusaidia kulinda maslahi ya Umma wa Kiislamu na kuimarisha nafasi yake dhidi ya changamoto za pamoja.

Kwa upande wake, al-Hayya amesifu uwezo wa Iran wa kusimama kidete dhidi ya vitisho, akisema nchi hiyo imebadilisha mlinganyo wa nguvu katika eneo la Maghariibi mwa Asia. Al-Hayya ameelezea matumaini yake kuwa Hamas inaweza kunufaika na uzoefu wa Iran katika mchakato wa mazungumzo ili kusaidia kulinda maslahi ya wananchi wa Palestina.