Iran yakanusha madai kuwa imeishambulia UAE kwa makombora
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i140786-iran_yakanusha_madai_kuwa_imeishambulia_uae_kwa_makombora
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha vikali madai ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwamba Iran imevurumisha makombora mawili ya balestiki kuelekea nchi hiyo.
(last modified 2026-08-19T05:53:24+00:00 )
Aug 19, 2026 04:18 UTC
  • Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei
    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha vikali madai ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwamba Iran imevurumisha makombora mawili ya balestiki kuelekea nchi hiyo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, amezionya nchi za kanda hii dhidi ya kutoa shutuma zisizo na msingi, huku akisisitiza umuhimu wa kuwa macho dhidi ya historia ya “operesheni za upotoshaji” (false-flag operations) ambazo zinalenga kuiingizia pande zisizo na hatia.

Katika matamshi yake siku ya Jumanne, afisa huyo alikanusha kabisa madai kuwa Iran ilirusha kombora lolote kuelekea UAE huku akilaani  vikali shutuma hizo zisizo na ukweli.

Amesisitiza kuwa tabia kama hiyo inakinzana na kanuni za ujirani mwema na inahujumu juhudi zinazoendelea za kujenga kuaminiana kati ya nchi za kanda hii, na kuzuia kuongezeka kwa ukosefu wa usalama.

Msemaji huyo pia ametoa wito kwa mataifa ya kanda hii kuzingatia changamoto na utata unaotokana na “vitendo viovu” vinavyoendelezwa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya amani na usalama wa kikanda.

Katika muktadha huu, Baghaei ameashiria historia ya idadi kubwa ya “operesheni za upotoshaji” na amezitaka nchi za kanda hii kujiepusha na kutoa shutuma zisizo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Jana Jumanne, Wizara ya Ulinzi ya UAE ilidai kuwa mifumo yake ya ulinzi wa anga ilikuwa “imegundua makombora mawili ya balestiki yaliyovurumishwa kutoka Iran kuelekea nchi hiyo.”

Siku hiyo hiyo ya Jumanne, mwandishi wa Press TV alifichua kuwa ripoti zinazodai Iran ilianzisha mashambulizi ya makombora dhidi ya UAE hazina msingi wowote.

Mwandishi huyo alijaribu kutofautisha madai hayo ya makombora ya Jumanne na mashambulizi ya kulipiza kisasi ambayo Iran imekuwa ikiyakiri hapo awali, yakilenga maslahi ya kijeshi ya Marekani katika kanda hii, kama jibu kwa uchokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Kulingana na mwandishi huyo, msimamo wa Iran katika kipindi chote cha uhasama huu umekuwa ni kutoa taarifa rasmi inapotekeleza hatua kama hizo za kulipiza kisasi.

Onyo la Baghaei lilikuja siku moja baada ya shambulio la droni kulenga ofisi ya Waziri Mkuu wa Mkoa wa Kurdistan nchini Iraq, Masrour  Barzani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alilaani shambulio hilo katika chapisho lake kwenye mtandao wa X, akisema: “Hakuna kinachohalalisha shambulio dhidi ya ofisi ya Waziri Mkuu Barzani. Marafiki zetu Wakurdi wanapaswa kuwa waangalifu dhidi ya operesheni za upotoshaji zinazolenga kupanda mbegu za chuki kati ya majirani.”

Aliongeza: “Tuliwalinda marafiki zetu Wakurdi dhidi ya dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein, na kundi la kigaidi la DAESH, na tunashukuru kwa usalama wao katika mpaka wetu.”