Niger yateua mkuu mpya wa majeshi baada ya jaribio la uasi lililozimwa
Serikali ya kijeshi ya Niger imemteua mkuu mpya wa jeshi, kufuatia jaribio la uasi wa jeshi lililozimwa mwezi uliopita. Hayo ni kwa mujibu taarifa iliyotolewa na televisheni ya taifa.
"Kupitia amri iliyotiwa saini mnamo Septemba 11, 2026, Jenerali Abdourahamane Tiani amemteua Brigedia Jenerali Mamane Sani Kiaou kuwa mkuu wa wafanyakazi wa jeshi," imetangaza televisheni ya taifa ikinukuu taarifa rasmi.Kiaou, ambaye hapo awali aliwahi kuwa mkuu wa jeshi la nchi kavu, anachukua nafasi ya Jenerali Moussa Salaou Barmou.Hata hivyo, taarifa hiyo haikueleza sababu za Barmou kuondolewa katika wadhifa wake.Kwa mujibu wa televisheni ya taifa ya Niger, Jenerali Tiani amemteua pia Jenerali Abdourahmane Abou Zataka kuchukua nafasi ya Kiaou kama mkuu wa jeshi la nchi kavu.Akielezewa na wenzake kama "kamanda mwenye uzoefu," Kiaou ameongoza mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi katika eneo la Tillaberi magharibi mwa Niger na eneo la Diffa kusini-mashariki mwa nchi hiyo.Kiaou aliongoza pia mazungumzo yaliyopelekea kuondolewa kwa vikosi vya Ufaransa na Marekani nchini Niger kufuatia mapinduzi ya Julai 2023.Itakumbukwa kuwa mnamo Agosti 29, wanajeshi walioasi katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi walishambulia uwanja wa ndege na ikulu ya rais katika mji mkuu, Niamey.Milipuko na milio ya risasi ilisikika pia katika kambi ya jeshi la anga, lakini jeshi la Niger lilifanikiwa kudhibiti tena eneo hilo na kuhitimisha uasi huo.
Baada ya kuingia madarakani, serikali ya Niger ilikata uhusiano wa kijeshi na Ufaransa na Marekani na kuimarisha uhusiano wake na Russia. Niger imeishutumu Ufaransa kwa kuwa nyuma ya uasi wa mwezi uliopita. Soumana Boubacar, msemaji wa serikali ya Niger, katika taarifa iliyosomwa kwenye televisheni, alisema kuwa uasi huo “ulichochewa na kuendelezwa na mtandao mpana wa njama ulioongozwa na utawala wa Kifaransa wa [Emmanuel] Macron.” Kinyume chake, Niger imeishukuru Russia, Algeria, na washirika wake katika eneo la Sahel, Burkina Faso na Mali, kwa kusaidia kuzima uasi.
Mvutano kati ya Niger na Ufaransa umekuwa ukiongezeka tangu mapinduzi ya mwaka 2023. Tangu wakati huo, Niger imeamuru kuondolewa kwa takriban wanajeshi 1,500 wa Ufaransa, imemfukuza balozi wa Ufaransa, kuzitimua kampuni za Ufaransa zinazochimba madini ya urani nchini humo, na pia kusimamisha matangazo ya vituo vinavyofadhiliwa na serikali ya Ufaransa, kama vile France 24 na RFI.