Jeshi la Niger lakamata silaha baada ya kuzima uasi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141182-jeshi_la_niger_lakamata_silaha_baada_ya_kuzima_uasi
Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Niger vimekamata hazina kubwa ya silaha na vifaa vya kijeshi baada ya kuzima uasi katika Kituo cha 101 huko Niamey, mji mkuu wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
(last modified 2026-09-10T06:05:36+00:00 )
Sep 04, 2026 03:14 UTC
  • Jeshi la Niger lakamata silaha baada ya kuzima uasi

Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Niger vimekamata hazina kubwa ya silaha na vifaa vya kijeshi baada ya kuzima uasi katika Kituo cha 101 huko Niamey, mji mkuu wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi hiyo, malori 34 aina ya Toyota yenye silaha zilizofichwa, magari mawili mepesi ya kivita (moja likiwa limeharibiwa), pikipiki kadhaa, silaha na vifaa vinginevyo, ni miongoni mwa vitu vilivyokamatwa katika operesheni hiyo.

Kwa upande wake televisheni ya taifa ya Niger nayo imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, kikundi kiitwacho Vives de la Nation, ambacho kinawakilisha sekta mbalimbali za jamii, kiliitisha mkutano maalumu siku ya Jumatano mjini Niamey ambao ulihudhuriwa na wanachama wa Baraza la Taifa la Ulinzi wa Nchi, maafisa wa serikali na maelfu ya wananchi kujadili suala hilo.

Waandaaji walisema kwamba mkutano huo uliitishwa ili kuonesha uungaji mkono kamili kwa serikali na viongozi wazalendo wa nchi hiyo na kuunga mkono kujitolea kwao katika kupingania uhuru na maendeleo ya taifa zima la Niger.

Wizara ya Ulinzi ya Niger ilitangaza Jumamosi kwamba ilikuwa imezima jaribio la uasi lililohusisha kundi moja la wanajeshi katika Kituo cha Anga cha 101 huko Niamey.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, kundi la wanajeshi "ambao walikuwa wamevunja nidhamu na kanuni za kijeshi" walijaribu kuwakamata baadhi ya wanajeshi wenzao katika kambi hiyo na kufyatua risasi katika maeneo kadhaa nyeti ya mji mkuu.

Hata hiyo radiamali na mwitikio wa haraka wa vikosi vya ulinzi na usalama vya Niger ulidhibiti haraka uasi huo, kuviwezesha vikosi hivyo kudhibiti hali ya mambo na kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote husika.