Makumi ya askari wakamatwa au kuuawa Niger baada ya jaribio la uasi
Baada ya karibu saa 24 za machafuko, makumi ya askari wamekamatwa au kuuawa katika mji mkuu wa Niger, Niamey kufuatia jaribio la uasi lililofanywa na askari wa jeshi la nchi hiyo.
Imeripotiwa kuwa uasi huo uliandaliwa na wanajeshi vijana waliokasirishwa na kushadidi kwa machafuko yanayosababishwa na wanamgambo chini ya serikali ya sasa ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa wachambuzi na wanadiplomasia, kikosi cha Russia cha Askari wa Afrika kilitoa msaada wa angani na nchi kavu kwa vikosi vya ndani ili kukabiliana na uasi huo.
Televisheni ya serikali ya Niger, RTN imeonyesha picha za makumi ya wanajeshi, wengi wao wakiwa vijana, wakiendeshwa gwaride hadharani baada ya milio ya risasi na miripuko kusikika usiku kucha katika kambi muhimu ya kijeshi.
Kambi hiyo iko ndani ya uwanja wa ndege wa mji mkuu Niamey na karibu na ikulu ya rais. Haijajulikana wazi mahali alipo kiongozi wa kijeshi Abdourahamane Tchiani.
Wachambuzi na wanadiplomasia wanasema, wanajeshi waasi walikuwa wamepiga kambi kwenye kambi ya kijeshi hadi Jumamosi jioni huku walinzi wa rais wakilinda ikulu ya rais na kupelekwa kurejesha udhibiti wa kambi hiyo.
Mara tu mazingira yaliporejea katika hali ya kawaida, mamia ya watu walikusanyika mjini Niamey kuonyesha uungaji mkono wao kwa kiongozi wa nchi hiyo, Abdourahmane Tiani.
Ibrahim Boubacar ambaye ni mkuu wa jumuiya inayounga mkono serikali amesema, "hatukubali kwamba watu wenye nia mbaya wajaribu kutuvuruga, au wajaribu kudhoofisha mchakato huu wa ukombozi ambao tumeukumbatia. Kwa sababu maadui wa nje tuliowatimua wameapa kuchukua hatua zote za lazima kutuvuruga na kuzusha mgawanyiko baina yetu".
Tiani aliingia madarakani katika mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2023 ambayo alisema yalichochewa na kushindwa serikali kukomesha vurugu za makundi ya waasi.
Tangu wakati huo, Niger imekata uhusiano na washirika wa usalama wa muda mrefu wa Magharibi, na badala yake imeigeukia Russia.
Hata hivyo machafuko yanayosababishwa na wanamgambo na mauaji yanayoshamiri ya askari wa vikosi vya usalama yameendelea kushuhudiwa, na kuripotiwa kuchochea machafuko ndani ya jeshi…/