Mgomo wa wauguzi Kenya waendelea kusababisha maafa, makumi ya wagonjwa wafariki mahospitalini
Wagonjwa wanawake wapatao 22 wameaga dunia kutokana na matatizo yanayohusiana na uzazi katika kipindi cha wiki moja katika hospitali za Kenya huku mgomo wa wauguzi ukiwa unaendelea.
Aidha, vifo vya watoto wachanga 44 na vifo 130 vya watoto kabla au wakati wa kuzaliwa pia vimeripotiwa, hali inayofichua ukubwa wa janga la afya linaloikumba nchi hiyo.
Takwimu hizo zimetolewa wakati wauguzi wakiwa wamesusia kazi kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa, hatua ambayo imevuruga huduma katika hospitali nyingi za umma kote nchini.
Wataalamu wa afya wanaonya kuwa, hali inaweza kuwa mbaya zaidi iwapo madaktari nao watatekeleza tishio lao la kugoma katika siku chache zijazo.
Mgomo wa wauguzi ulianza Julai 29, kufuatia mzozo kuhusu utekelezaji wa Mkataba wa Pamoja wa Kazi wa mwaka 2017, marupurupu mbalimbali na kuajiriwa kwa wahudumu wa mpango wa Afya kwa Wote (UHC) kwa masharti ya kudumu.
Kaunti za Nakuru, Kisumu, Kakamega na Kajiado zimetajwa kuwa miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi na mgomo huo.
Hospitali ambazo awali zilikuwa zikihudumia mamia ya wagonjwa kila siku, sasa zimebaki na shughuli chache huku wagonjwa wakikosa huduma muhimu.
Baadhi ya familia zimewahamishia wagonjwa wao kwenye hospitali za binafsi kwa hofu ya kupoteza maisha.
“Tumeamua kumtoa mgonjwa wetu hospitalini kwa sababu hajapata matibabu ya maana kwa wiki tatu. Tunampeleka hospitali ya binafsi kwa matumaini ya kupata huduma bora,” ameeleza mmoja wa jamaa za mgonjwa.
Huku mazungumzo kati ya viongozi wa Chama cha Wauguzi na Baraza la Magavana yakikosa kuzaa matunda, wananchi wanaendelea kulipa gharama kubwa zaidi.
Wengi wanasema serikali za kaunti na serikali kuu zimekuwa zikilaumiana huku maisha ya wagonjwa yakiendelea kuwa hatarini.
Hofu kubwa iliyopo hivi sasa ni kwamba, iwapo mgomo huo utaendelea kwa muda mrefu zaidi, vifo vitaongezeka; na hospitali za umma, ambazo ndizo tegemeo la mamilioni ya Wakenya maskini, zitaendelea kuwa maeneo ya mateso badala ya vituo vya kuokoa maisha…/