Araqchi: Iran haina uadui na nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi
-
Sayyid Abbas Araqchi
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema jibu la Iran la kushambulia kambi za kijeshi za Marekani katika baadhi ya nchi za Ghuba ya Uajemi halina maana kwamba Iran inashambulia nchi hizo.
Sayyid Abbas Araqchi amesema hayo katika mazungumzo yake na mwenzake wa China, Wang Yi. Amesisitiza kwamba Iran haina uadui wa aina yoyote na nchi za Ghuba ya Uajemi na ina azma thabiti ya kudumisha uhusiano wa ujirani mwema na nchi hizo.
Araqchi amesema kuwa: Jibu la Iran la kushambulia kambi za kijeshi za Marekani katika baadhi ya nchi za Ghuba ya uajemi halipaswi kutambuliwa kuwa ni mashambulizi dhidi ya nchi hizo, bali ni jibu halali dhidi ya chanzo cha uchokozi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Marekani na Israel zimevunja sheria na vigezo vyote vya kimataifa kwa kuishambulia Iran na kwamba hadi sasa mamia ya raia wasio na hatia yoyote wameuawa shahidi katika mashambulizi hayo.
Amesema vikosi vya ulinzi vya Iran vimeazimia ipasavyo kulinda mamlaka ya kitaifa, ardhi na usalama wa raia wa Jamhuri ya Kiislamu.