IRGC: Majibu yajayo yatakuwa makali zaidi, Tel Aviv yateketea kwa makombora
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137130-irgc_majibu_yajayo_yatakuwa_makali_zaidi_tel_aviv_yateketea_kwa_makombora
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema, kiwango cha nguvu za makombora kitaongezwa na mwendelezo wa mashambulio dhidi ya maadui wavamizi utazidi kurefushwa.
(last modified 2026-03-03T14:10:15+00:00 )
Mar 03, 2026 14:06 UTC
  • IRGC: Majibu yajayo yatakuwa makali zaidi, Tel Aviv yateketea kwa makombora

Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema, kiwango cha nguvu za makombora kitaongezwa na mwendelezo wa mashambulio dhidi ya maadui wavamizi utazidi kurefushwa.

Brigedia Jenerali Ali Mohammad Naeini ameeleza hayo siku ya Jumanne alipozungumzia mwendelezo wa mashambulizi ya kijeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia Operesheni ya Ahadi ya Kweli 4 na kusisitiza kwamba, majibu ya siku ya kwanza na ya pili ya vita yalikuwa ya nguvu kubwa zaidi na ya kuteketeza zaidi kuliko ya siku za mwishoni mwa vita vya siku 12; na makombora yaliyotumika yameboreshwa zaidi na yamekuwa ya kisasa zaidi kuliko yalivyokuwa katika Operesheni ya Ahadi ya Kweli 3.

Wakati huohuo, Idara ya Uhusiano wa Umma ya IRGC imeeleza katika taarifa nambari 13 ya Operesheni ya Ahadi ya Kweli 4 kwamba, katika wimbi la 14 la Operesheni ya Ahadi ya Kweli 4, vikosi vya wanamaji vya Jeshi hilo la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu alfajiri ya kuamkia Jumanne vimefanya shambulizi kali la makombora na ndege zisizo na rubani lililolenga kituo cha anga cha jeshi la Marekani kilichoko katika eneo la Sheikh Isa nchini Bahrain. Shambulio hilo lililohusisha droni 20 na makombora matatu limelenga shabaha kwa umakini na kuliteketeza kikamilifu jengo kuu la kamandi na makao makuu ya kituo cha anga cha Marekani.

Hayo yamejiri katika hali ambayo, licha ya uchujaji mkubwa wa habari unaofanywa na utawala wa kizayuni wa Israel, duru za upashaji habari kutoka Tel Aviv zimeripoti kuwa makombora ya Iran yamefanikiwa kupiga maeneo yaliyokusudiwa ya utawala huo. Ripoti zinasema, makombora ya vikosi vya ulinzi vya Iran yamelenga maeneo ya Raasul-A’ain na Patkh Tikwa mjini Tel Aviv…/