Wabunge wa Marekani: Netanyahu amemtwisha Trump mpango wake dhidi ya Iran
-
Seneti ya Marekani
Mtandao wa The Hill umewanukuu wabunge waandamizi wa vyama vyote viwili vikubwa vya Marekani, Democtatic na Republican, wakisema kuwa uamuzi wa Donald Trump wa kuanzisha vita dhidi ya Iran umechukuliwa kutokana na imla ya mpango wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Mtandao wa Hill umeandika kuwa, maafisa wa ngazi za juu wa serikali wamesema katika kikao cha ripoti ya siri cha Kongresi ya Marekani kilichowashirikisha wabunge wa Domocratic na Republican kwamba mpango wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuishambulia Iran umeilazimisha Marekani kufanya mashambulizi eti ya kujikinga kwa kisingizio cha kuwalinda askari na wanajeshi wa Marekani waliopo Magharibi mwa Asia.
Mark Warner, seneta Mdemocrat na Naibu Mkuu wa Kamati ya Ujasusi ya Seneti ya Marekani amesema katika kikao hicho kwamba uamuzi wa kuanzisha mashambulizi makubwa ya kijeshi dhidi ya nchi nyingine kwa sababu tu ya mashinikizo ya muitifaki wa Marekani unaisukuma nchi kuelekea kusikojulikana.