Kenya yaisitisha ujenzi wa kituo cha Ebola cha Marekani
-
Picha ya setilaiti kituo cha karantini cha Ebola cha Marekani katika Kambi ya Jeshi ya Laikipia katika Kaunti ya Laikipia, nchini Kenya, Juni 22
Wizara ya Afya ya Kenya imesitisha ujenzi wa kituo cha karantini cha ugonjwa wa Ebola kinachozua utata, ambacho kinamilikiwa na Marekani, baada ya changamoto ya kisheria kuhoji uhalali wa mradi huo na hatari zake kwa jamii.
Hatua hiyo imekuja baada ya Waziri wa Afya, Aden Duale, kufika mbele ya Mahakama Kuu jijini Nairobi na kuomba msamaha kwa kukaidi amri ya awali ya mahakama iliyokuwa imetaka ujenzi wa kituo hicho cha karantini kusimamishwa. Siku moja kabla, mnamo Jumatatu, waziri huyo alipatikana na hatia ya kuidharau mahakama katika uamuzi uliotolewa na Jaji wa Mahakama Kuu, Patricia Nyaundi.
Katika taarifa, wizara hiyo imesema, “Waziri pia aliihakikishia mahakama kuwa ujenzi na shughuli zote katika eneo hilo zimesimamishwa kikamilifu, na akaelezea masikitiko yake kwa kutoelewana au dhana yoyote ya kutotii amri za mahakama."
Jaji Nyaundi alimuonya Duale dhidi ya kukaidi maelekezo ya mahakama tena na akamwachilia bila kumpa adhabu yoyote.
Kituo hicho cha karantini kilichopendekezwa katika Kambi ya Jeshi ya Laikipia iliyoko Nanyuki, takriban kilomita 200 kaskazini mwa Nairobi, kilizua mjadala mwezi uliopita baada ya Marekani kutangaza mpango wa dola milioni 13.5 ili kuimarisha kile kinachotajwa kuwa ni utayari wa Kenya kukabiliana na Ebola, kufuatia mlipuko mbaya wa ugonjwa huo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Marekani ilikuwa inapanga kutumia kituo hicho cha karantini kwa ajili ya raia wake wanaotoka Kongo, jambo ambalo limekosolewa vikali na Wakenya wanaona hatua hiyo kama mpango wa Marekani wa kuitumia nchi hiyo kama jaa la taka.
Taasisi ya Katiba (Katiba Institute), shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake Nairobi, iliwasilisha ombi mahakamani mwezi Mei, ikibainisha kuwa mradi huo unaweza kuleta hatari ya kiafya kwa umma katika nchi ambayo haijawahi kurekodi kesi hata moja ya Ebola.
Wataalamu wa afya nchini Marekani, wakiwemo maafisa wa zamani kutoka Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), wameonya kuwa mradi huo unaleta “changamoto kubwa za kitabibu, kimaadili, kiutendaji, na kisheria.”
Takriban watu watatu waliripotiwa kuuawa mapema mwezi huu wakati wa maandamano dhidi ya mpango huo huko Nanyuki.
Mnamo Mei 28, Mahakama Kuu ya Nairobi iliizuia serikali ya Kenya kuendelea na ujenzi huo hadi hapo ombi lililowasilishwa na Taasisi ya Katiba litakapotatuliwa.
Licha ya amri hiyo, imebainika kuwa ndege zilizobeba vifaa vya matibabu na wataalamu zimeendelea kutua katika kambi hiyo ya kijeshi.
Siku ya Jumanne, Waziri wa Afya wa Kenya, Duale, aliambia mahakama kuwa maamuzi yaliyofanywa na Wizara ya Afya “yanaongozwa na ushahidi wa kisayansi, ushauri wa kitaalamu, na mikakati ya afya ya umma.” Hata hivyo, ameema kuwa “ushirikiano uliopendekezwa” kati ya Nairobi na Washington kuhusiana na kituo hicho ulisimamishwa “mara tu baada ya amri za mahakama kutolewa.”