Mlipuko wa Ebola Kongo wapindukia maambukizi 4,000
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140490-mlipuko_wa_ebola_kongo_wapindukia_maambukizi_4_000
Idadi ya kesi za Ebola zilizothibitishwa hadi kufikia jana Ijumaa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zilikuwa zimepindukia 4,000 huku maeneo ya afya yaliyoathirika yakiongezeka.
(last modified 2026-08-08T02:46:46+00:00 )
Aug 08, 2026 02:42 UTC
  • Mlipuko wa Ebola Kongo wapindukia maambukizi 4,000

Idadi ya kesi za Ebola zilizothibitishwa hadi kufikia jana Ijumaa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zilikuwa zimepindukia 4,000 huku maeneo ya afya yaliyoathirika yakiongezeka.

Mlipuko wa hivi karibuni wa Ebola nchini Kongo unatajwa kuwa mlipuko wa pili kwa ukubwa duniani kwa idadi ya maambukizi yaliyorekodiwa.

Ripoti ya karibuni ya hali ya mambo ya Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeeleza kuwa nchi hiyo imeripoti jumla ya wagonjwa 4,053, vikiwemo vifo 1,850, tangu mlipuko huo ulipotangazwa rasmi nchini hum katikati ya mwezi wa Mei mwaka huu.

 

Mlipuko wa virusi vya Bundibugyo umeathiri maeneo 53 ya afya katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Haut-Uele na Tshopo.

Ituri, kitovu cha mlipuko huo, inachangia asilimia 86.9 ya wagonjwa wa Ebola waliothibitishwa.

Mamlaka za afya nchini Kongo zimeeleza kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini iwapo mabadiliko katika virusi hivyo yanaweza kuwa yanachangia kueneza zaidi maambukizi.

Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC), Jean Kaseya juzi Alhamisi waliwaeleza waandishi wa habari kwamba idadi ya maambukizi na watu waliopoteza maisha kwa Ebola nchini Kongo inaweza ikawa ya chini.

Kaseya ametoa wito kwa jami kuwa mstari wa mbele, ametaka kuwepo ufuatiliaji zaidi wa watu waliotangamana na wagonjwa, na kurahisisha upatikanaji wa vipimo na huduma za matibabu.