Wabunge Kenya: Hakuna makubaliano mapya ya ushirikiano wa kijeshi na Uingereza
-
Wanajeshi wa Uingereza walioko Kenya.
Wabunge wa Kenya wamesema kuwa hakuna makubaliano mapya yaliyofikiwa kati ya Kenya na Uingereza kuhusu mkataba wa ushirikiano wa kijeshi (BATUK).
Kauli hiyo imetolewa baada ya Uingereza kudai kuwa kumekuwa na maendeleo makubwa katika kutekeleza baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi.
Uingereza ilisema maafisa wake wakuu walikutana na maafisa wa serikali ya Kenya, wabunge na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Masuala ya Kigeni mwezi Juni mwaka huu kujadili hatua iliyofikiwa.
Uingereza pia imesema taratibu za pamoja za kushughulikia mabomu na vilipuzi ambavyo havijalipuka zimekamilishwa.
London pia imesema imeweka hatua mpya za kuzuia unyanyasaji wa kingono unaofanywa na na wanajeshi wa kikosi cha Uingereza wanaopata mafunzo Kenya (BATUK) katika Kaunti ya Laikipia.
Hata hivyo, Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi iliambia Bunge Jumanne iliyopita kuwa mkataba huo bado haujaidhinishwa.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Nelson Koech, alisema makubaliano hayo hayawezi kuanza kutumika hadi masharti yaliyowekwa na Kenya yatimizwe.
Bw Koech alisema kamati haitakubali mkataba unaokiuka Katiba au kudhalilisha Wakenya.
Siku chache zilizopita ripoti ya siri ya Polisi ya Kenya ilifichua madai mazito ya ubakaji, ulawiti wa watoto na ukiukaji wa haki za kibinadamu unaodaiwa kufanywa na wanajeshi wa kikosi cha Uingereza wanaopata mafunzo Kenya (BATUK) katika Kaunti ya Laikipia.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Mei 19, 2026, iliyotiwa saini na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na kuwasilishwa bungeni, baadhi ya wanajeshi wa Uingereza walivuka kutoka eneo lao la mazoezi ya kijeshi hadi vijiji jirani na kuwashambulia raia.
Katika Kaunti ya Laikipia pekee, polisi wa Kenya walirekodi visa vya watu 37 waliodaiwa kubakwa na genge la wanajeshi wa Uingereza, watu 20 kubakwa na wengine wawili kujeruhiwa walipokuwa wakijaribu kutoroka mashambulizi hayo.
Wabunge wa Kenya wanataka makubaliano ya mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya nchi hiyo na Uingereza yafanyiwe marekebisho ili kosa la mauaji lisikilizwe katika mahakama za Kenya, na BATUK iwajibike zaidi kupitia miradi ya uwajibikaji kwa jamii.