Kamanda: Jeshi la Iran bado halijaonesha uwezo wake kamili
-
Brigedia Jenerali Ahmadreza Pourdastan
Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yamebadili mwelekeo wa kimkakati kutoka kwenye ulinzi pekee na kuelekea kwenye mafundisho ya kijeshi ya mashambulizi (offensive military doctrine), huku operesheni za kutangulia kumzuia adui (preemptive operations) zikiwa sasa mezani.
Hayo ni kwa kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Ahmadreza Pourdastan, Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Onyo hilo linaashiria kuwa Iran bado haijatumia sehemu kubwa ya uwezo wake wa kijeshi katika uwanja wa mapambano.
Brigedia Jenerali Pourdastan ameyasema hayo katika mahojiano na Shirika la Habari la Fars siku ya Jumanne, akitoa tathmini ya msimamo wa kijeshi wa Iran na mabadiliko ya usawa wa nguvu katika kanda ya Asia Magharibi
Amesema kama italazimu, Jeshi la Iran linaweza kumshangaza adui vibaya kupitia operesheni za kutangulia kumzuia adui katika nyanja ambazo hazijui.”
Kamanda huyo amesisitiza kuwa majeshi ya Iran yako katika utayarifu wa hali ya juu na bado hayajaonesha uwezo wao wote. “Majeshi bado hayajatumia sehemu kubwa ya uwezo wao,” amesema Brigedia Jenerali Pourdastan akiongeza kuwa adui anajua vyema kuwa makosa yoyote ya mahesabu yatajibiwa kwa hatua zitakazovuka “mipaka na Lango Bahari la Hormuz.”
Akiashiria utendaji wa Iran katika vita vya hivi karibuni vya siku 12 na siku 40, Jenerali Pourdastan amesema Jamhuri ya Kiislamu na Mhimili wa Muqawama umefanikiwa katika vita “visivyo na usawa” dhidi ya muungano wa “Mayahudi, Magharibi na Waarabu” unaoongozwa na Marekani.
Ametaja ombi la adui la kusitisha mapigano kama ishara kuu ya ushindi. “Katika historia ya vita, upande unaoomba kusitisha mapigano daima ni ule unaoelekea kushindwa,” amesema Pourdastan, akielezea matamshi ya hivi karibuni ya Marekani kama ishara ya kukata tamaa badala ya kuwa kielelezo cha nguvu.
Akizungumzia hali tete nchini Lebanon, Jenerali huyo wa Jeshi la Iran amethibitisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kuwalinda wananchi wa Lebanon. Amesema kuwa majeshi ya Iran yamekaribia mara kadhaa kuingia vitani na utawala wa Israel katika mwezi uliopita.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, vitisho vya Iran viliilazimisha Marekani kuishinikiza Israel kusitisha uchokozi wake kusini mwa Lebanon ili kuzuia mzozo mpana zaidi.