Rais wa Somalia: Tutazuia Israel kuimarisha ushawishi wake Somaliland
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140388-rais_wa_somalia_tutazuia_israel_kuimarisha_ushawishi_wake_somaliland
Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, amesema kwamba Serikali ya Shirikisho itachanganya "nguvu na hekima" ili kuzuia "Israel" kupata nafasi au kuanzisha ushawishi wa kudumu katika eneo la "Somaliland," akisisitiza kwamba Mogadishu ingali inashikamana na umoja wa ardhi na mamlaka ya Somalia, na inapinga kwa nguvu zote kuhamisha migogoro ya "Mashariki ya Kati" hadi eneo la Pembe ya Afrika.
(last modified 2026-08-03T11:13:55+00:00 )
Aug 03, 2026 11:10 UTC
  • Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud
    Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud

Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, amesema kwamba Serikali ya Shirikisho itachanganya "nguvu na hekima" ili kuzuia "Israel" kupata nafasi au kuanzisha ushawishi wa kudumu katika eneo la "Somaliland," akisisitiza kwamba Mogadishu ingali inashikamana na umoja wa ardhi na mamlaka ya Somalia, na inapinga kwa nguvu zote kuhamisha migogoro ya "Mashariki ya Kati" hadi eneo la Pembe ya Afrika.

Katika hotuba yake mbele ya Bunge la Shirikisho, Sheikh Mahmoud amesema kwamba serikali inatumia zana zote za kidiplomasia, njia za ushirikiano wa kimataifa na mikakati ya kitaifa kulinda mamlaka ya nchi na kuzuia majaribio yoyote ya kutishia usalama wake, akibainisha kuwa msimamo wa Somalia umesisitizwa katika majukwaa mbalimbali ya kikanda na kimataifa.

Katika muktadha huo, amesisitiza kwamba nchi yake haitaruhusu migogoro inayoendelea katika eneo la "Mashariki ya Kati" kupanuliwa hadi Pembe ya Afrika, ikizingatiwa kwamba hilo ni tishio la moja kwa moja kwa usalama na utulivu wa kikanda. Ameongeza kuwa kuhamisha mgogoro na mashaka yanayoshuhudiwa "Mashariki ya Kati" kwa karibu karne moja sasa hadi Pembe ya Afrika "ni jambo lizilokubalika kabisa, na halina maslahi yoyote kwa watu wa Somalia au watu wa kanda hii."

Kuhusu mustakabali wa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia na changamoto zinazohusiana na kupungua misaada ya kimataifa, rais wa Somalia amesisitiza kwamba nchi yake ina uwezo unaohitajika wa kijeshi na kwamba vikosi vya majeshi ya Somalia vina uwezo wa kutimiza majukumu yao ya usalama. Hayo yamekuja huku kukiwepo majadiliano kuhusu mustakabali wa Ujumbe wa Msaada na Kuimarisha Utulivu wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (AUSSOM).

Mnamo Desemba 26, 2025, Israel ilitangaza kutambua rasmi Somaliland kama nchi inayojitawala. Serikali ya Somalia ilipinga vikali uamuzi huo wa Israel, ikiutaja kuwa ni "hatua haramu na shambulio la makusudi dhidi ya mamlaka, umoja wa ardhi ya Somalia, na mipaka inayotambuliwa kimataifa" ya nchi hiyo.

Israel inafanya mikakati ya kuimarisha ushawishi wake katika Lango Bahari la Bab al-Mandab na eneo la Pembe ya Afrika kama sehemu ya mkakati mpana wa kiusalama na kisiasa.