Changamoto mpya kwa Wasaudia kufuatia mzingiro wa majini wa Yemen
Mzingiro wa majini wa Yemen dhidi ya Saudi Arabia, pamoja na kufungwa kwa Lango-Bahari la Bab al-Mandab kwa meli za mafuta za Saudia, vimetoa changamoto mpya kwa Wasaudia.
Mnamo tarehe 20 Julai 2026, Jeshi la Yemen lilitangaza rasmi mzingiro wa majini dhidi ya Saudi Arabia. Hatua hiyo ilichukuliwa kwa ajili ya kujibu mashambulizi ya anga ya Saudia dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Sana'a na mzingiro wa miaka kumi na miwili unaoendelea dhidi ya Yemen, jambo lililochochea mvutano kufikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tena tangu kusainiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano mwaka 2022. Hatua hiyo ilipiga marufuku usafiri wa majini kwa Saudia kwa kuzingatia kanuni ya "mzingiro kwa mzingiro," na hivyo kuisababishia Riyadh matatizo makubwa yasiyo na mfano wake.
Kufungwa kwa Lango-Bahari la Bab el-Mandeb kwa meli za mafuta za Saudia kumeongeza gharama ya kusafirisha mafuta ya nchi hiyo katika masoko ya kimataifa, na kuzilazimisha meli hizo kuzunguka bara zima la Afrika ili kufikia masoko ya barani Asia.
Zaidi ya hayo, tofauti na miaka ya 1970 na 1980, wakati wanunuzi wakuu wa mafuta ya Saudia walikuwa Ulaya na Marekani, leo wengi wa wanunuzi wa mafuta ya nchi hiyo wako Asia Mashariki, hasa China. Ni wazi kuwa mabadiliko haya ya njia ya uchukuzi yamekuwa changamoto kubwa kwa Riyadh. Mbali na ukweli kwamba meli za kubeba mafuta ghafi ya Saudi Arabia sasa zinalazimika kusafiri kwa muda mrefu zaidi ili kuzunguka bara zima la Afrika, gharama za usafirishaji pia zimepanda. Kwa mfano, gharama ya kusafirisha mafuta kwa meli kutoka bandari ya Yanbu iliyo Bahari ya Shamu hadi Taiwan imeongezeka kwa zaidi ya dola milioni moja.
Suala jingine linahusu usafirishaji wa mizigo ya meli hizo kupitia Mfereji wa Suez. Katika muktadha huu, kampuni ya utafiti ya Energy Aspects imeripoti kuwa meli kubwa hulazimika kupita kwenye mfereji huo zikiwa na mzigo pungufu kutokana na vikwazo vilivyowekwa, na hatimaye kuchukua sehemu iliyosalia ya mzigo wao katika Bahari ya Mediterania.
Ni wazi kuwa mzingiro wa majini uliotangazwa na Yemen unatoa tishio la moja kwa moja kwa njia muhimu za usafiri wa baharini kwa Saudi Arabia. Lango-Bahari la Bab el-Mandeb, ambalo asilimia 12 ya biashara ya dunia hupitia humo, liko katikati ya mvutano huu. Bomba la mafuta la "Mashariki-Magharibi" ambalo husafirisha zaidi ya mapipa milioni 7 ya mafuta kwa siku kutoka mashariki mwa Saudi Arabia hadi bandari ya Yanbu iliyoko katika Bahari ya Sham, linakabiliwa na hatari kubwa. Mzingiro huo unakwenda sambamba na hatua ya Iran ya kufunga Lango-Bahari la Hormuz, jambo linaloifanya Saudi Arabia kukosa njia mbadala za uchukuzi wa baharini.
Ni wazi kuwa mzingiro huo wa Yemen umesababisha madhara makubwa kwa uchumi wa Saudi Arabia. Ripoti zinaonyesha kuwa njia mbadala huongeza gharama ya takriban dola 9 kwa kila pipa la mafuta, hali inayotoa mashinikizo makubwa ya kifedha katika bajeti ya Saudi Arabia na hivyo kupunguza uwezo wa mafuta ya nchi hiyo kushindana katika soko la dunia. Gharama za mafuta kwa kila meli ya kubeba mafuta zimepanda kutoka takriban dola milioni 1.26 hadi dola milioni 2.87; ikijumuisha ada za Mfereji wa Suez, ambapo gharama ya kila safari imeongezeka kwa takriban dola milioni 2.5.
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limetabiri kuwa ukuaji wa uchumi wa Saudi Arabia kwa mwaka huu wa 2026 utakuwa kwa karibu asilimia 2 pekee. Wataalamu wa uchumi wanakadiria kuwa iwapo mzingiro huo utaendelea, bei ya mafuta itapindukia dola 150 kwa pipa. Hadi sasa, meli 16 za Saudi Arabia zimelazimika kusimamisha safari zao, ambapo kwa uchache meli tatu za kubeba mafuta zimeshambuliwa, jambo linaloonyesha mafanikio ya mzingiro wa majini wa Yemen. Wakati huo huo, Wayemen wamezidisha mashambulizi yao ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya taasisi za mafuta za Aramco huko Yanbu na Jizan, pamoja na mji wa Jizan kusini mwa Saudi Arabia. Kiwanda cha kusafisha mafuta cha Jizan kimeshambuliwa na kuteketezwa, jambo lililosababisha uharibifu mkubwa katika sehemu muhimu ya kiwanda hicho. Mifumo ya ulinzi wa anga ya Saudia ilizuia makombora ya balistiki yaliyolenga viwanda vya kusafisha mafuta vya Yanbu, hali inayoashiria tishio kubwa kwa miundombinu muhimu ya nchi hiyo.
Hali hii ya uhasama inajitokeza wakati ambapo Saudi Arabia imekuwa ikijitahidi kuepuka kurejea vitani nchini Yemen tangu mwaka 2022; hata hivyo, sasa inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kimkakati, kijeshi, kiuchumi na kisiasa. Hivyo, tunapasa kusema kuwa mzingiro wa majini wa Yemen umebadilisha hali ya kimkakati ya eneo na kuiweka Saudi Arabia katika hali ngumu isiyo na mfano wake. Riyadh, ambayo ndiyo iliyoanzisha mzingiro huo, sasa inakabiliwa na matokeo mabaya ya hatua hiyo hiyo. Kuendelea kwa hali hii kunaweza kuibua mgogoro mkubwa zaidi wa nishati, kuongezeka kuyumba kwa masoko ya mafuta duniani pamoja na kuongezeka mivutano katika eneo. Suluhisho la mgogoro huu ni zaidi ya hatua za kijeshi, ambapo linahitajia tathmini ya kina kuhusu sera za hujuma na uadui za Saudi Arabia dhidi ya Yemen na udharura wa nchi hiyo ya kifalme ambayo ni kibaraka wa Magharibi, kukubali kuhitimisha mzingiro wa miaka kumi na miwili dhidi ya watu wa Yemen kwa msingi wa uadilifu na uzingatiaji wa haki za msingi za taifa la Yemen.