Pezeshkian: Kuwajibika kwa Marekani ndio sharti la kuendelea mazungumzo
-
Rais Masoud Pezeshkian
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametilia mkazo umuhimu wa kutekelezwa makubaliano yaliyofikwa baina ya Iran na Marekani kwa ajili ya kuendelezwa mazungumzo kati ya pande hizo kuhusu utekelezaji wa mkataba wa maelewano uliosainiwa hivi karibuni.
"Ufanisi wa mazungumzo unategemea kushikamana kikamilifu na majukumu yaliyokubaliwa na utekelezaji wake sahihi," ameandika Rais Pezeshkian katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X leo Jumanne.
"Maendeleo katika njia hii yatapimwa kwa kuzingatia kushikamana kivitendo na majukumu yaliyoainishwa," amesema Rais Masoud Pezeshkian na kuongeza: "Matamshi yanayotolewa nje ya yaliyomo katika hati ya makubaliano hayasaidii kuendeleza mazungumzo."
Matamshi hayo yamekuja huku maafisa wa Marekani, akiwemo Rais Donald Trump, wakitoa maoni mara kwa mara kuhusu wigo unaodaiwa wa mazungumzo hayo na maudhui yake.
Jamhuri ya Kiislamu imepinga mara kwa mara matamshi hayo yasiyo na tija, ikipuuza madai ya kukubali vifungu vilivyo nje ya wigo wa hati ya maelewano yenye vifungu 14.
Hati hiyo ya maelewano ilisainiwa hivi karibuni na marais wa Iran na Marekani kwa lengo la kukomesha uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, ambao ulianza kulenga Jamhuri ya Kiislamu mnamo Februari 28.