Kwa nini Ulaya ina wasiwasi kuhusu mrengo wa Lebanon?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i139330-kwa_nini_ulaya_ina_wasiwasi_kuhusu_mrengo_wa_lebanon
Uungaji mkono wa Ulaya juu kwa usimamishaji hujuma ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon katika maelewano kati ya Tehran na Washington unaonyesha wasiwasi unaoongezeka wa nchi za Ulaya kuhusu kuenea vita na taathira zake hasi katika uthabiti na usalama wa eneo.
(last modified 2026-06-22T05:57:44+00:00 )
Jun 22, 2026 05:52 UTC
  • Kwa nini Ulaya ina wasiwasi kuhusu mrengo wa Lebanon?

Uungaji mkono wa Ulaya juu kwa usimamishaji hujuma ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon katika maelewano kati ya Tehran na Washington unaonyesha wasiwasi unaoongezeka wa nchi za Ulaya kuhusu kuenea vita na taathira zake hasi katika uthabiti na usalama wa eneo.

Kansela wa Ujerumani Friedrich Mertz amesema: "Sote tunakubali kwamba sasa ni muhimu kwamba usitishaji vita ulioanzishwa kati ya Marekani na Iran udumishwe pia kusini mwa Lebanon." Kauli hii ya Friedrich Mertz labda ndiyo ishara muhimu zaidi ya mabadiliko ya kimtazamo ya Ulaya kuhusu matukio ya Asia Magharibi baada ya shambulio la pili la Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ukweli kwamba kiongozi wa nchi ambayo daima imekuwa mmoja wa waungaji mkono wakuu wa utawala wa Kizayuni barani Ulaya sasa anasisitiza ulazima wa kuenezwa usitishaji vita kati ya Tehran na Washington hadi Lebanon si tu msimamo wa kidiplomasia, bali unaakisi uelewa mpya wa hali halisi ya kijiopolitiki ya eneo; ukweli ambao kwa msingi wake usalama wa Lebanon hauzingatiwi tena kama suala la pembeni, bali ni sehemu ya mipango mipya ya usalama wa kikanda.

Kadhalika, uungaji mkono wa Ulaya wa kujumuisha usitishaji uchokozi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon katika hati ya maelewano ya Tehran-Washington unaweza kutathminiwa kabla ya jambo jingine lolote kuwa unatokana na wasiwasi wa kudhoofishwa utaratibu uliowekwa baada ya vita. Viongozi wa Ulaya wanajua vizuri kwamba iwapo utawala ghasibu wa Israel utadumisha uwanja wa vita wa Lebanon, kiutendaji kipengele kimojawapo cha maelewano kati ya Iran na Marekani kitakuwa kimekiukwa na hivyo kuhatarisha utaratibu mzima wa kumaliza vita. Kwa mtazamo huu, Lebanon imekuwa kipimo cha kupima kiwango cha uwajibikaji wa Marekani kuhusu makubaliano hayo na kudumishwa usitishaji vita katika nyanja zote. Ulaya pia imegundua kuwa vita vya Asia Magharibi haviwezi tena kubakia katika eneo moja la kijiografia. Uzoefu wa miezi iliyopita umeonyesha kwamba hatua yoyote ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni inaweza kuchochea mlolongo wa hatua za kulipiza kisasi katika ngazi ya kieneo. Shambulio dhidi ya Lebanon, tofauti na siku za nyuma, halitamaanisha tu makabiliano kati ya utawala wa Israel na Hizbullah, bali kuna hatari kwamba wahusika wengi wa kieneo wataingizwa tena kwenye mzozo huo, na hivyo kuibua mgogoro mpya kuanzia Mashariki ya Mediterania hadi Bahari Nyekundu na Ghuba ya Uajemi. Ulaya, kwa kutilia maanani kuwa bado inakabiliwa na matokeo hasi ya vita vya Ukraine, mashinikizo ya kiuchumi na migogoro ya usalama, haiwezi tena kumudu hali nyingine ya mivutano mikubwa ya kijeshi.

Wakati huo huo, suala la usalama wa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa kusini mwa Lebanon pia ni muhimu sana kwa Wazungu. Ufaransa, Italia na Uhispania ndio wachangiaji wakuu wa kikosi cha UNIFIL, na kuanza tena uhasama wowote kunaweza kuhatarisha moja kwa moja maisha ya wanajeshi wa Ulaya walioko kusini mwa Lebanon. Kushindwa ujumbe wa UNIFIL pia kunaweza kudhoofisha imani si tu kwa Umoja wa Mataifa, bali pia kwa Umoja wa Ulaya kama mojawapo ya waungaji mkono muhimu wa operesheni za kulinda amani kimataifa.

Kauli ya Meretz, kama ilivyo ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, ni muhimu sana kwa mtazamo mwingine. Ikiwa kufikia karibuni hivi, ukosoaji wa sera za Israel ulikuwa ukitolewa zaidi na nchi chache za Ulaya kama Uhispania na Ireland, lakini sasa viongozi wa madola mawili makuu ya Umoja wa Ulaya nao wanatahadharisha kuhusu matokeo ya tabia ya baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu. Sisitizo la Macron kuhusu kutokubalika kwa hali ya hivi sasa ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na uungaji mkono wake kwa juhudi za kuwekekwa vikwazo mawaziri wa Israel wenye itikadi kali, pamoja na wito wa Meretz wa kuzuia kuongezeka mivutano, ni mambo yanayoonyesha kuwa hata washirika wa jadi wa Tel Aviv wanahofia sera zinazoweza kulisukuma eneo kwenye vita visivyoisha. Ujumbe muhimu zaidi wa kauli hizi ni kukubalika kimyakimya ukweli kwamba hakuna mpango endelevu wa usalama katika eneo unaweza kufikiwa bila kuzingatiwa nafasi ya Iran. Uungaji mkono wa Ulaya kwa kifungu kinachoashiria kusitishwa operesheni za kijeshi nchini Lebanon ndani ya fremu ya maelewano ya Tehran-Washington, kwa hakika, ni kukiri ukweli kwamba Iran imekuwa moja ya pande kuu za mlingano wa usalama wa eneo, na kwamba kupuuzwa ukweli huu hakutachangia uthabiti wa Lebanon wala kudhamini usalama wa eneo pana la Asia Magharibi. Kwa hiyo, uungaji mkono wa Ulaya kwa ajili ya kuingizwa Lebanon katika mkataba wa maelewano wa Iran na Marekani, kabla ya jambo lolote, ni juhudi za kuhifadhi makubaliano yanayoweza kuzuia eneo kurudi tena kwenye mzunguko wa vita, kuzuia chokochoko zaidi za Netanyahu, na kutoa fursa ya kuundwa kwa utaratibu mpya wa usalama katika eneo; ambao, tofauti na siku za nyuma, utasimama kwenye msingi wa kuzingatia ukweli wa nguvu halisi katika eneo na ulazima wa kushirikishwa wachezaji wote wenye ushawishi katika eneo.