Araqchi: Mwenendo wa wanadiplomasia wa Ufaransa Tehran haukubaliki
-
Sayyid Abbas Araqchi azungumz akwa simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amelaani mwenendo wa wanadiplomasia wawili wa Ufaransa mjini Tehran na kuutaja kuwa "usiokubalika," huku akiitaka Paris kuzuia kujirudia vitendo vinavyokwenda kinyume na taratibu za kidiplomasia.
Araghchi aliibua suala hilo katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot, jana Jumanne walipojadili matukio ya karibuni ya pande mbili, ya kikanda na ya kimataifa.
Araghchi alilalamikia mwenendo "usio wa kawaida" wa wanadiplomasia hao wawili wa Ufaransa, akisema kuwa vitendo vyao haviendani na viwango vinavyokubalika vya kidiplomasia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia alieleza kuwa kwa kuzingatia sheria na kanuni za nchi mwenyeji, pamoja na kanuni za kidiplomasia zinazotambulika kimataifa, ni muhimu balozi za kigeni kuendelea kufanya kazi katika uda wa diplomasia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amehihimiza z serikali ya Ufaransa kuchukua hatua zinazohitajika ili kuzuia kukaririwa matukio kama haya.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Ufaransa wamezungumza kwa njia ya simu kufuatia kauli zilizotolewa Jumatatu na Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, aliyedai kuwa wanadiplomasia wao wawili mjini Tehran walizuiliwa na kutendewa vibaya. Barrot alidai kuwa wanadiplomasia hao walikuwa na jukumu la kukuza mabadilishano ya kitamaduni na umma pamoja na jamii ya wasomi nchini Iran.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa pia jana ilimwita Kaimu Balozi wa Iran mjini Paris kuhusiana na tukio hilo.