Kwa nini Israel haina uwezo wa kuilazimisha Hizbullah ijisalimishe?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i139318-kwa_nini_israel_haina_uwezo_wa_kuilazimisha_hizbullah_ijisalimishe
Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya nchini Lebanon amesema, maadui walijaribu kuandaa mazingira ya kuuangamiza muqawama kwa kutumia vibaya serikali ya Lebanon na kuunda mwavuli haramu wa kisheria, lakini pamoja na hayo si tu kwamba adui wa Kizayuni alishindwa kuilazimisha Hizbullah ijisalimishe, bali pia inaendelea kupipigania ushindi wa mwisho.
(last modified 2026-06-21T14:17:08+00:00 )
Jun 21, 2026 12:42 UTC
  • Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah
    Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah

Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya nchini Lebanon amesema, maadui walijaribu kuandaa mazingira ya kuuangamiza muqawama kwa kutumia vibaya serikali ya Lebanon na kuunda mwavuli haramu wa kisheria, lakini pamoja na hayo si tu kwamba adui wa Kizayuni alishindwa kuilazimisha Hizbullah ijisalimishe, bali pia inaendelea kupipigania ushindi wa mwisho.

Swali ni je, licha ya mashambulizi makali ya mabomu ya miaka mitatu iliyopita, kwa nini hadi sasa Israel imeshindwa kuilazimisha Hizbullah ijisalimishe?

Swali hili linapasa kujibiwa katika mtazamo wa uwezo wa kijeshi, kisiasa, kijamii na kiitikadi wa Hizbullah nchini Lebanon. Kwa mtazamo wa uwezo wa Hizbullah, suala la kwanza ni la kidini na kiimani. Hizbullah ni harakati muhimu nchini Lebanon ambayo ina misingi ya kiimani na kidini nchini humo. Msingi huu wa kidini na kiitikadi umejikita katika mwamko wa Ashura na uzingatiaji wa mafundisho yanayotokana na hamasa ya Karbala ya Imam Hussein (as), mjukuuu wa Mtume Mtukufu (saw) na Imam wa tatu wa Shia, ambaye hajisalimishi mbele ya ukandamizaji na dhulma ya wazi. Itikadi hii anakichukulia kifo cha ushahidi kuwa heshima ya hali ya juu. Kuhusiana na hilo, Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema: "Adui wa imani hajashinda uimara wetu na kuendelea kuwepo uwanjani. Sisi tupo kwenye medani ya vita na tunastahimili matatizo na vikwazo vyote. Sisi ni kundi ambalo haliogopi kifo na sisi ni washindi daima katika kukabiliana na wale wanaotutishia kifo. Maadamu tutaendelea kufuata misingi hii chini ya anwani ya "Hussein ni njia yetu," kila hatua inayochukuliwa katika njia ya kukabiliana na uvamizi inachukuliwa kuwa ushindi kwetu."

Suala la pili linahusu muundo na uwezo wa kijeshi wa Hizbullah nchini Lebanon. Hizbullah ni mchezaji na vuguvugu la muundo thabiti nchini Lebanon ambao haujasimama kwenye msingi wa watu binafsi. Mauaji ya kigaidi ya makamanda wake hayatapelekea Hizbullah kuporomoka kimuundo. Pamoja na hayo, Hizbullah imekuwa ikijiandaa kwa vita vya muda mrefu kwa miaka mingi. Kuundwa kwa mtandao madhubuti wa mahandaki na kambi za kijeshi za chini ya ardhi kusini mwa Lebanon kunafanya iwe vigumu sana kwa jeshi lolote lile, hata liwe na ubora wa aina gani wa anga, kutambua na kushambulia vikosi vyake pamoja na mitambo ya kurushia makombora. Miundombinu hii inaruhusu vikosi vya Hizbullah kuepuka mashambulizi ya anga ya adui na kudumisha uwezo wake wa kurusha makombora.

Suala la tatu ni ushawishi wa Hizbullah katika matabaka ya kijamii ya nchi na kunufaika kwake na mtaji wa kijamii. Maana ya "matabaka ya kijamii" katika kuchambua uwezo wa Hizbullah ni kwamba kundi hili sio jeshi kama majeshi mengine ya kawaida, bali linafungamana kikamilifu na muundo wa jamii ya Lebanon, haswa kusini mwa nchi. Kwa hiyo, harakati kama hii iliyo na uungaji mkono mkubwa wa wananchi na iliyo na imani thabiti ya kidini haiwezi kujisalimisha kirahisi kupitia ulipuaji wa mabomu. Kwa hivyo ni kutokana na sifa hizi za kidini, kijeshi na kijamii ndio maana utawala wa Kizayuni haujaweza kuitishia Hizbullah na kuifanya ijisalimishe mbele ya mabomu na makombora katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Mabomu na makombora yanaweza kudhoofisha nguvu ya kijeshi, lakini hayawezi kuharibu "utambulisho wa kijamii na kidini" ambao umejikita katika matabaka ya kina ya jamii ya Lebanon. Kuendelea mashambulizi ya kinyama ya Israel dhidi ya Hizbullah, hasa dhidi ya raia wa kawaida wakiwemo watoto na wanawake kutazidisha tu jinai na hatimaye kupelekea kushindwa kwa utawala huo wa Kizayuni.