Mamilioni ya Wairani washiriki maombolezo kuelekea siku ya Ashura
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i139396-mamilioni_ya_wairani_washiriki_maombolezo_kuelekea_siku_ya_ashura
Mamilioni ya Waislamu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na maeneo mengine ya dunia leo mchana wameshiriki katika maombolezo ya kumbukumbu ya Ta'asua na jioni hii wanashiriki katika hafla za mkesha wa Ashura ambayo ni kukumbuka siku ya kuuliwa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (AS).
(last modified 2026-06-24T11:14:30+00:00 )
Jun 24, 2026 11:04 UTC
  • Mamilioni ya Wairani washiriki maombolezo kuelekea siku ya Ashura

Mamilioni ya Waislamu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na maeneo mengine ya dunia leo mchana wameshiriki katika maombolezo ya kumbukumbu ya Ta'asua na jioni hii wanashiriki katika hafla za mkesha wa Ashura ambayo ni kukumbuka siku ya kuuliwa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (AS).

Ashura ni mwezi 10 Mfunguo Nne, Muharram, ambayo mwaka huu imesadifiana na Alhamisi  tarehe 15 Juni, 2026.

Imam Husain (AS) aliuawa shahidi kikatili na kinyama mwaka wa 61 Hijria katika jangwa la Karbala nchini Iraq baada ya kuongoza mapambano ya kishujaa ya ushindi wa damu mbele ya upanga.

Marasimu ya Muharram hushika kasi zaidi tarehe 9 na 10 Mfunguo nne ambapo mamilioni ya Waislamu kutoka maeneo mbalimbali ya dunia huwasili katika mji mtakatifu wa Karbala kwa ajili ya maombolezo na kukumbuka tukio chungu la kuuawa shahidi Imam Hussein (AS).

Waombolezaji hapa nchini Iran wakiwa wamevaa nguo nyeusi, kama ishara ya huzuni na majonzi, walikuwa wakibubujikwa na machozi kwa kukumbuka dhulma iliyofanywa na madhalimu dhidi ya Imam Hussein (AS), watu wa nyumba yake na wafuasi wake watiifu. Aidha mwaka huu maadhimisho hayo yana muelekeo wa kipekee baada ya vita vya siku 40 vya kichokozi Marekani na Israel dhidi ya Iran ambavyo vilianza tarehe 10 Ramadhani sawa na Februari 28.

Wananchi wanaoshiriki katika hafla za maombolezo mwaka huu wameapa kufungamana na malengo matukufu ya Kiongozi Muadhamu aliyeuawa shahidi vitani Imam Khamenei (MA). Aidha wametangaza kumtii kikamilifu Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyeteuliwa Ayatullah Mujtaba Khamenei

Wanaoshiriki katika maombolezo husikiliza qiraa ya Qur'ani Tukufu, hotuba na mashairi kuhusiana na masaibu yaliyomkumba Imam Hussein AS huko Karbala.

Mapambano ya Karbala ya Imam Hussein (AS) na wafuasi wake watiifu yalitokea mwaka 61 Hijria, na watukufu hao walipigana kishujaa katika vita vya kidhulma dhidi ya maelfu ya wanajeshi wa khalifa wa Bani Umayyah, Yazid mwana wa Muawiya, mwana wa Abu Sufyan ambaye alikuwa adui mkubwa wa Mtume Muhammad (SAW) na Waislamu na ambaye alitambulika kwa ulevi na kucheza kamari.

Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote na kwa kila mpenda haki na ukombozi duniani kwa mnasaba wa kukumbuka msiba huu adhimu.