Mazishi ya Imam Khamenei kufanyika kwa siku sita nchini Iran na Iraq
-
Shahidi Imamu Khamenei
Makao makuu ya kumbukumbu ya Kiongozi aliyeuawa shahidi wa Iran, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei yametangaza ratiba ya mazishi ya siku sita katika miji mitano, ikianza na shughuli ya kuaga mwili wake kwa siku mbili mjini Tehran mnamo Julai 4 na kumalizika kwa maziko yake katika mji mtakatifu wa Mash'had, tarehe 9 Julai.
Mazishi ya Imam Ali Khamenei na watu kadhaa wa familia yake waliouawa katika mashambulizi ya kushtukiza ya Marekani na Israel Februari 28 dhidi ya nyumba yake mjini Tehran yataanza na shughuli ya kuaga mwili wake katika Ukumbi wa Grand Imam Khomeini Mosalla mjini Tehran Jumamosi, Julai 4, na Jumapili, Julai 5.
Shughuli kuu ya mazishi hayo mjini Tehran imepangwa kufanyika Jumatatu, Julai 6, ambapo miili ya mashahidi wengine wanne—Dk. Mesbahul-Huda Baqeri (mkwe), Sayyidah Bushra Husseini Khamenei (binti), Zahra Haddad Adel (mkamwana), na Zahra Mohammadi Golpaygani (mjukuu)—itasindikizwa pamoja na Kiongozi aliyeuawa shahidi wa Iran.
Siku ya Jumanne, Julai 7, shughuli ya mazishi itafanyika katika mji mtakatifu wa Qum, ambapo mwili wa Imam Khamenei utaswaliwa Swala ya Maiti.
Kisha msafara huo utasafirishwa hadi Iraq siku ya Jumatano, Julai 8, kufuatia maombi ya mara kwa mara ya makabila, wasomi, watu mashuhuri, wanasiasa na viongozi wa kidini wa Iraq.
Marasimu ya mazishi itafanyika katika miji mitakatifu ya Najaf na Karbala, baada ya serikali ya Iraq kutangaza nyakati na maeneo maalumu.
Kamati ya maandalizi ya shughuli hiyo imetoa shukrani kwa mamlaka ya kidini ya Iraq, serikali na wananchi kwa maombi yao ya kufanyika shughuli ya mazishi ya Imam Ali Khamenei katika maeneo matakatifu huko Najaf al Ashraf na Karbala al Muqaddasa.
Maziko ya Ayatullah Ali Khamenei yamepangwa kufanyika Alhamisi, Julai 9—sambamba na usiku wa kuuawa shahidi Imam Ali bin Hussein Sajjad (as) —katika Haram ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Ali bin Musa al Ridha huko Mash'had.
Msemaji wa kamati ya maandalizi ya shughuli hiyo pia ametangaza kwamba wajumbe rasmi, wanasiasa na wasomi kutoka kote duniani watatoa heshima kwa mwili wa Kiongozi shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, baada ya maelezo ya muda na mahali pa kufanyia mkutano kutolewa na Wizara ya Mambo ya Nje.
Kauli mbiu ya ukumbusho wa tukio hilo ni "Lazima Tusimame" ikiambatana na ngumi iliyokunjwa kama ishara yake. Katika nchi za Kiarabu, kauli mbiu rasmi itakuwa " قوموا لله" (Simameni kwa Ajili ya Mungu).
Ayatallah Ali Khamenei, pamoja na wanafamilia kadhaa, waliuawa shahidi Februari 28 katika uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.