Jumanne, 24 Februari, 2026
Leo ni Jumanne 6 Ramadhani 1447 Hijria ambayo inasadifiana na 24 Februari 2026.
Leo tarehe 5 mwezi wa Esfand kwa kalenda ya Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi na kumkumbuka mwanafikra mkubwa wa Kiislamu na Kiirani, Khajah Nasiruddin Tusi.
Sikuu hii inajulikana pia katika kalenda ya Iran kwa jina la Siku ya Uhandisi.
Abu Jaafar Muhammad bin Muhammad maarufu kwa jila na Khajah Nasiruddin Tusi aliyepewa laqabu ya "mwalimu wa wanadamu" na Muhaqqiq Tusi alizaliwa mwaka 597 Hijria katika eneo la Tusi kaskazini mashariki mwa Iran. Katika kipindi cha maisha yake, mwanafalsafa, mwanahisabati, mnajimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiirani aliasisi kituo kikubwa cha kielimu na akademia ya kwanza ya sayansi yaani mahala pa kufuatilia mwenendo wa nyota, mwezi na jua iliyojulikana kwa jina la Maraghe huko kaskazini magharibi mwa Iran. Aalimu huyo aligundua namna mpya za kutumia saa ya jua kwa ajili ya kituo hicho. Kituo hicho kilikuwa na suhula muhimu zaidi ambazo hazikushuhudiwa katika nchi za Magharibi kwa kipindi cha miaka 300 baada yake.
Vilevile alikusanya vitabu vya elimu na taaluma mbalimbali kutoka Iraq, Sham, kaskazini mwa Afrika na maeneo ya kandokando mwa Iran na kuasisi maktaba kubwa iliyokuwa na zaidi ya vitabu laki nne.
Khajah Nasiruddin Tusi alifariki dunia mwaka 672 Hijria akiwa na umri wa miaka 75 na kuzikwa katika mji wa Kadhimain nchini Iraq. ***
Miaka 492 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Luis Vaz de Camoens, malenga mkubwa wa Kireno na mmoja wa wanafasihi wakubwa wa Ulaya huko Lisbon mji mkuu wa Ureno.
Mbali na kuwa mshairi, De Camoens alikuwa mpiganaji jasiri. Moja ya kazi muhimu za utunzi za Luis Vaz de Camoens ni ile aliyoipa jina la" The Lusiads." ***
Miaka 178 iliyopita katika siku kama ya leo utawala wa muda au duru ya pili ya mfumo wa jamhuri ulianza huko Ufaransa baada ya wananchi kufanya mapambano ya ukombozi na kumuondoa madarakani Luis Phillipe Mfalme mbeberu wa nchi hiyo.
Utawala wa aina hiyo unajulikana pia katika historia ya Ufaransa kwa jina la "Utawala wa Waandishi wa Habari". Hii ni kwa sababu waandishi habari 11 waliokuwa wakipigania mfumo wa jamhuri chini ya uongozi wa Alphonse de Lamartine malenga na mwandishi wa Kifaransa, ndio waliokuwa wakisimamia utawala huo. ***
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita sawa na tarehe 24 Februari 1949 wawakilishi wa Misri na utawala wa Kizayuni wa Israel walisaini mkataba wa kusitisha mapigano kati ya pande mbili hizo huko katika kisiwa cha Rhodes kilichoko katika bahari ya Aegean.
Ni vyema kutaja hapa kuwa baada ya kuundwa serikali ya Kizayuni mwaka 1948 huko katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Misri ilishirikiana bega kwa bega na baadhi ya nchi za Kiarabu katika kupigana vita dhidi ya utawala wa Kizayuni.
Hata hivyo wanajeshi wa utawala huo walifanikiwa kuingia katika ardhi ya Misri na Lebanon baada ya kuishambulia safu ya vikosi vya mapambano vya Waarabu ambavyo vilikuwa na zana chache za kisasa za kivita na hivyo kutoa pigo kwa vikosi vya nchi za Kiarabu. ****