Kwa nini Marekani imeelekeza mashambulizi yake kusini mwa Iran?
Hatua ya majeshi ya Iran ya kudhihirisha nguvu moja kupitia operesheni madhubuti kama vile kufunga Lango Bahari la Hormuz, inatoa ujumbe kwa adui kwamba hakuna migawanyiko yoyote iliyopo jeshini katika uwanja wa vita na kwamba uwezo wote wa taifa umejikita katika lengo moja la kulinda maslahi ya taifa kwa gharama yoyote ile, dhidi ya adui Mmarekani na Mzayuni.
Katika mkutano wa mshikamano na mashauriano uliofanyika hivi karibuni kati ya makamanda wakuu wa Jeshi na Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC kwa lengo la kuimarisha shughuli za ulinzi wa taifa dhidi ya hujuma ya adui, pande hizo mbili zilibadilishana mawazo kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili kwa shabaha ya kukabiliana na uchokozi wa adui. Mojawapo ya mambo muhimu yaliyofikiwa katika kikao hicho ni tangazo la uungaji mkono wa wazi na mkubwa wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa jeshi la IRGC licha ya njama na hatua za uhasama za baadhi ya nchi za kuituhumu IRGC kuwa ni taasisi ya kigaidi, na hivyo kuonyesha tena umoja usiotetereka wa nguvu za kijeshi katika kulinda usalama wa nchi.
Mwishoni mwa kikao hicho, washiriki walisisitiza kwamba ujumbe muhimu zaidi wa kikao hicho ni kutilia mkazo umoja na mshikamano kati ya vikosi vyote vya kijeshi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mhimili wa "Uislamu, Mapinduzi na Taifa", ujumbe wa wazi unaoonyesha msimamo usioyumba wa vikosi hivi wa kulinda thamani na kuvunja propaganda za vyombo vya habari vya adui.
Kufungwa Lango-Bahari la Hormuz si uamuzi uliofanywa juzi au jana tu; Meja Jenerali Rahim Safavi, Msaidizi na Mshauri Mwandamizi wa Amiri Jeshi Mkuu, amesema, mnamo 2012, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, alitaka mpango madhubuti wa kufunga lango hilo uandaliwe kwa ushirikiano wa makamanda wakuu wa majeshi yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na baada ya kukamilika na kukabidhiwa kwa Kiongozi Muadhamu, aliuwasilisha kwa kamanda mkuu wa majeshi kwa ajili ya kutekelezwa wakati muafaka.
Hatua zote zinazoendelea kuchukuliwa katika Lango-Bahari la Hormuz, hususan baada ya vita vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, zinadhihirisha uwezo wa nchi hii wa kuzuia uchokozi wa adui (uwezo wa kuzuia hujuma). Uwezo wa kuzuia hujuma hutimia pale adui anapohitimisha kuwa gharama ya shambulio ni kubwa zaidi kuliko faida inayoweza kupatikana, ambapo ushirikiano wa nguvu za majeshi katika medani ya vita bila shaka huimarisha uwezo huo, jambo lililoonekana wazi katika vita vya siku 12 na siku 40, na sasa vya hivi sasa dhidi ya Iran. Ikumbukwe pia kuwa vitisho vingi duniani huishia kwenye makaratasi tu. Pale ushirikiano madhubuti wa vikosi vya kijeshi unapotekelezwa kivitendo, kama kufungwa Lango-Bahari, adui hutambua kuwa Iran ina uwezo na pia utashi wa dhati wa kutekeleza vitisho vyake. Uwiano huu wa tishio na hatua ya kivitendo ndiyo njia ya haraka zaidi inayovunja nguvu na nia ya adui.
Kwa kawaida, adui hupanga mikakati yake kwa kuzingatia udhaifu na migawanyiko ya ndani. Lakini baada ya kushuhudia nguvu ya pamoja inayoonyeshwa na upande wa pili (Iran) katika uwanja wa vita, hutambua kuwa kuna ushirikiano kamili, na hivyo kupelekea njama zake za kutaka kuibua migawanyiko jeshini au kuvuruga mipangilio miongoni mwa vikosi vya ulinzi kuambulia patupu. Katika vita viwili vya karibuni, lengo lilikuwa kuharibu uwezo wa kijeshi na makombora ya Iran. Lakini nini kilitokea? Kwa maneno ya Brigedia Jenerali Ibn al-Reza, Kaimu Waziri wa Ulinzi wa Iran: "Uzoefu wa vita vya karibuni umeonyesha kuwa sekta ya ulinzi ya Iran si tu haikusimama, bali kwa kutegemea maarifa ya ndani, inaendelea na safari yake ya kupiga hatua kubwa kiteknolojia kwa nguvu kubwa."
Hivyo, kushindwa huko kwa mahesabu kunamfanya adui ahitimishe kuwa makabiliano ya moja kwa moja na muundo kama huo kutampelekea ashindwe vibaya na kwa uchungu. Katika muktadha huu, mtu anapasa kujiuliza kuwa je: Kwa nini adui msaliti, baada ya kupuuza na kuvunja makubaliano ya Islamabad, sasa anashambulia kusini mwa Iran? Kwa nini hashambulii Tehran na mikoa mingine kama ilivyokuwa katika vita vingine viwili vya kulazimishwa? Jibu liko wazi: Anafahamu kuwa akipanua wigo wa uchokozi wake, atatumbukia katika kinamasi kirefu na kushindwa kujinasua; hivyo, ameridhika na kushambulia kusini mwa nchi kwa matumaini ya kufanikisha malengo yake. Karibuni hivi au baadaye, bila shaka atakumbwa na kushindwa tena. Kwa nini? Kwa sababu nguvu ya kuzuia hujuma inayotokana na ushirikiano wa majeshi ndicho kizuizi hasa kinachomrudisha nyuma adui. Adui anapoona kuwa akili ya kamandi na nguvu tendaji (yaani majeshi) vinafanya kazi kwa uwiano kamili na vina azimio lisilotikisika, huona kuwa njia pekee ya kujinasua kwenye kinamasi ni kubadilisha mkakati na kurudi nyuma, kwani anajua fika kuwa hakuna ushindi wa haraka unaoweza kupatikana dhidi ya mfumo madhubuti ulioungana na uliosimama imara.