Jul 16, 2026 03:15 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 16 Julai, 2026

Alkhamisi tarehe Mosi Safar 1448 Hijria, sawa na Julai 16 mwaka 2026.

Siku kama ya leo miaka 1411 iliyopita, awamu ya mwisho ya vita kati ya jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) na Muawiya bin Abi Sufiyan ilianza katika eneo la Siffin kandokando ya Mto Furati (Euphrates) nchini Iraq. Baada ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) kushika hatamu za uongozi Muawiya alikataa kumpa mkono wa utiifu na akaamua kuanzisha vita dhidi ya serikali yake.   ***

Tarehe Mosi Safar miaka 1387 iliyopita, msafara wa familia ya Mtume Muhammad (SAW) ambayo ilichukuliwa mateka katika vita vya Karbala, uliwasili katika eneo la Sham ambao ulikuwa makao makuu ya utawala wa Yazid bin Muawiya.

Wakiwa Sham, Ahlul Bait wa Mtume (SAW) hususan Bibi Zainab (as) na Imam Sajjad (as) walitoa hutuba tofauti katika msikiti wa Sham wakifichua maovu ya Yazidi, kiongozi dhalimu wa Bani Umayyah. Vilevile Ahlul Bait wa Mtume (SAW) walifikisha kwa watu ujumbe wa harakati ya mashahidi wa Karbala kwa njia nzuri kiasi kwamba watu wa Sham walielewa ukweli kuhusu jinai za jeshi la Yazid na kuzua hasira dhidi ya mtawala huyo.

Hali hiyo ilimfanya Yazidi aliyetoa amri ya kuuawa Imam Hussein (as) na wafuasi wake, akane uhakika huo na kumtwisha lawama hizo Ubaidullah bin Ziyad, aliyekuwa gavana wa mji wa Kufa, Iraq. ***

Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita James Parkinson aligundua ugonjwa wa Parkinson na namna unavyotokea.

Kwa sababu hiyo ugonjwa huo ulipewa jina la tabibu huyo. Dalili za ugonjwa huo ni kama vile kutetemeka sana na kwa muda mrefu kwa ulimi, kichwa na mikono na kushindwa kuvuta miguu wakati wa kutembea hususan katika kipindi cha uzeeni na pia kukakamaa misuli katika sehemu yoyote ya mwili.

Ugonjwa wa Parkinson unasababishwa na baadhi ya matatizo katika ubongo na hadi kufikia sasa hakuna dawa mujarabu iliyopatikana kwa ajili ya kutibu maradhi hayo.    ***

Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon kwa mara nyingine tena ilifanikiwa kupokea mateka watano na miili ya karibu mashahidi 200 wa Kilebanoni kutoka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ubadilishanaji huo wa miili na mateka hao ulifanyika kufuatia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya pande mbili hizo kwa usimamizi wa serikali ya Ujerumani.

Nukta ya kushangaza katika oparesheni hiyo ni kwamba vyombo vya usalama na ujasusi vya utawala wa Kizayuni hadi dakika ya mwisho havikuwa na habari kwamba wanajeshi wake wawili waliopangwa kukabidhiwa katika operesheni hiyo waliuawa mwanzoni mwa mapigano kati ya jeshi la utawala wa Kizayuni na wapiganaji wa Hizbullah.

Shakhsia wengine kutoka makundi ya mapambano ya Lebanon pia walikuwa miongoni mwa mateka walioachiwa huru na utawala wa Kizayuni. Shakhsia muhimu zaidi kuliko wote alikuwa Samir Qantar ambaye alipoteza karibu miaka 30 ya umri wake akiwa katika jela za utawala wa Kizayuni.    ***

Na katika siku kama hii ya leo miaka 11 iliyopita alifariki dunia qarii mashuhuri wa Misri, Sheikh Sayyid Mutawalli Abdul Aal.

Alizaliwa Aprili 1947 katika familia ya wachamungu nchini Misri na alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa na umri wa miaka 12.

Alianza kujifunza qiraa ya Qur'ani Tukufu kwa kuiga mitindo ya maustadhi bingwa kama vile Sheikh Abdulbasit Abdusamad na Sheikh Mustafa Ismail.

Katika umri wake uliojaa baraka za Qur'ani, Sayyid Mutawalli Abdul Aal alitembelea nchi nyingi duniani kama qarii na pia jaji wa mashindano ya Qur'ani. Alifariki dunia Julai 16, 2015 akiwa na umri wa miaka 68.