ElBaradei kwa Netanyahu: Umeiharibu Gaza, sasa unazungumzia "uhuru" wa watu wake!
Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) Mohamed ElBaradei, amemhutubu Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akisema: "Umeiharibu Gaza, na sasa unazungumzia uhuru wa watu wake!"
Mohamed ElBaradei amesisitiza kuwa: Israel imefanya uhalifu mkubwa kwa kuharibu Gaza na kuua makumi ya maelfu ya watu, lakini sasa inazungumzia "uhuru" wa watu wa eneo hilo kuondoka katika ardhi yao.
Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) ameendelea kwa kusema: "Uhalifu huo hauwezi kufikirika! Umeigeuza Gaza kuwa rundo la vifusi na kuua makumi ya maelfu ya watu. Sasa unazungumzia uhuru wa watu?!"
Mwanasiasa huyo wa Misri na mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, ametoa maoni hayo akijibu kauli za Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuhusu haki ya watu wa Gaza kuondoka katika eneo hilo.
Netanyahu, hapo awali alidai katika mahojiano na chombo cha habari cha Kiebrania kwamba: "Kuna sehemu mbili tu duniani ambazo watu hawawezi kuziacha. Korea Kaskazini na Gaza. Watu wa Gaza hawaruhusiwi kabisa kuondoka."
Netanyahu ambaye anauzingira Ukanda wa Gaza kwa zaidi ya miaka kumi sasa na anazuiya hata kuingia misaada na mahitaji muhimu ya binadamu kama dawa na maji, ameendelea kwa kudai: "Kwa nini watu wa Gaza wasiwe na haki sawa ya msingi - haki ya kuhama - ambayo mabilioni ya watu kote duniani wanafurahia?"
"Hii ni jinai kubwa ambayo haiwezi kufikirika! Umeigeuza Gaza kuwa rundo la vifusi, ukaua makumi ya maelfu ya watu, na sasa unazungumza na kutetea "uhuru" wa watu wake wa kuondoka katika ardhi yao!," amehoji Dakta Mohamed ElBaradei.