Jumanne tarehe 4 Agosti 2026
-
Leo Katika Historia
Leo ni tarehe 20 Safar 1448 Hijria sawa na Agosti 4 mwaka 2026.
Leo Jumanne inasadifiana na mwezi 20 Mfunguo Tano Safar 1448 Hijria, siku ya kumbukumbu ya 40 ya mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW, Imam Husain AS ambaye pia ni Imam wa Tatu wa Waislamu.
Siku kama ya leo miaka 1387 iliyopita, ilifanyika majlisi ya kwanza ya siku ya Arubaini tangu kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein bin Ali (as) na watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume ambao waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria.
Majlisi ya siku ya Arubaini hufanyika kila mwaka baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume na masahaba zake watiifu ambao walijisabilia roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika ardhi ya Karbala.
Imam Husain AS na wafuasi wake 72 waliuliwa kidhulma na kikatili katika jangwa la Karbala huko Iraq mwaka wa 61 Hijria.
Idadi kubwa ya Waislamu na wafuasi wa dini nyinginezo kwa miaka mingi huwa wanatembea kwa miguu kuanzia siku chache kabla ya 40 ya Imam Husain AS, kutoka mji wa Najaf kwa ajili ya kwenda kufanya ziara katika Haram na bwana huyo wa mashahidi huko Karbala. ****
Miaka 234 iliyopita alizaliwa Percy Bysshe Shelley malenga wa Uingereza.
Percy alianza kupenda taaluma ya fasihi tangu utotoni na kuonyesha kipawa kikubwa katika uwanja huo. Alikuwa mfuasi na muungaji mkono wa thamani za upendo, urafiki na uhuru na sababu hiyo ndiyo iliyomfanya avutiwe na Mapinduzi ya Ufaransa ambayo ndio kwanza yalikuwa yametokea.
Percy Bysshe Shelley aliaga dunia mwaka 1822 akiwa na umri wa miaka 30 baada ya boti yake kuzama katika Bahari ya Mediterrania. ***
Miaka 221 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa William Rowan Hamilton mwanahisabati na mtaalamu wa elimu ya fizikia wa Ireland.
Alikuwa na kipaji cha hali ya juu kiasi kwamba akiwa na umri wa miaka 13 alikuwa amejifunza lugha 12 za dunia zikiwemo Kiarabu na Kifarsi. William Rowan Hamilton talivutiwa sana na elimu za fizikia na hisabati na alifanikiwa kuanzisha baadhi ya kanuni na mifumo muhimu katika elimu hizo. Akiwa na umri wa miaka 22 Hamilton alikuwa tayari mwalimu wa elimu ya nujumu. Msomi huyo aliaga dunia 1865.
Katika siku kama ya leo miaka 151 iliyopita, aliaga dunia Hans Christian Andersen mwandishi wa vitabu vya watoto wa nchini Denmark.
Alizaliwa mwaka 1805 na tangu akiwa mdogo alikuwa na mapenzi makubwa na visa. Baada ya kuaga dunia baba yake, Hans Christian Andersen akiwa na umri wa miaka 11 aliacha shule na kuanza kufanya kazi. Baada ya kuingia katika maonyesho na michezo ya kuigiza ya kifalme, hali yake ya maisha iliboreka na hivyo akaamua kuendelea na masomo.
Mwandishi huyo wa Kidenmark awali alianza kujihusisha na utungaji mashairi na kuandika visa na simulizi. Hata hivyo baadaye Andersen aliondokea kuwa na mapenzi makubwa na visa vya watoto na alionyesha kipaji kikubwa alichokuwa nacho katika uwanja huo. ****
Siku kama ya leo miaka 133 iliyopita, alizaliwa Ayatullahil-Udhma Mar’ashi Najafi mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu katika mji wa Najaf nchini Iraq.
Baba yake ni Sayyid Shamsuddin Mahmoud Mar’ashi aliyekuwa miongoni mwa wanazuoni na mafaqihi wakubwa katika zama zake. Baada ya kukamilisha masomo ya awali na ya Kiislamu huko Najaf, Mar’ashi Najafi alianza kuhudhuria darsa na masomo ya Usul kwa Agha Dhiyau Iraqi na Sheikh Ahmad Kashif al-Ghitaa.
Ayatullah Mar’ashi Najafi alipata daraja ya juu ya elimu ya Ij’tihad akiwa na umri wa miaka 27.
Mojawapo ya kazi kubwa zilizofanywa na mwanazuoni huyo mkubwa ni "Maktaba ya Ayatullah Mar'ashi", ambayo ilianzishwa katika mji wa Qum mnamo 1344 kwa gharama ya kibinafsi ya Ayatullah Marashi Najafi. Maktaba hiyo kwa sasa ina zaidi ya vitabu 250,000 vilivyochapishwa na vitabu 31,000 vilivyoandikwa kwa hati za mkono. Ayatullah Mar'ashi Najafi alifariki dunia tarehe 7 Safar 1411 katika mji wa Qum. ****
Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, vikosi vilivyokuwa na mrengo wa utaifa nchini Uturuki vikiongozwa na Mustafa Kemal Ataturk vilianza kuwashambulia wanajeshi wa Ugiriki waliokuwa wameikalia kwa mabavu nchi hiyo.
Baada ya kusambaratika utawala wa Othmania katika Vita vya Kwanza vya Dunia, ardhi asili ya utawala huo yaani Uturuki iliangukia mikononi mwa tawala waitifaki. ****
Katika siku kama ya leo miaka 96 iliyopita, alizaliwa Ayatullah Sayyid Ali Sistani faqihi, alimu na marjaa taqlidi wa Kislamu katika mji wa Mash'had, Iran.
Alianza kujifunza Qur'ani akiwa na miaka 5, na akiwa na umri wa miaka 11 alianza kusoma masomo ya kidini ya utangulizi baada ya kutakiwa na baba yake kufanya hivyo. Baadaye alielekea katika mji wa Qum kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Ayatullah Sistani alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini mjini Najaf, Iraq hapo baadaye.
Hii leo Ayatullah Ali Sistani si tu kwamba, anahesabiwa kuwa marjaa mkubwa zaidi nchini Iraq bali pia amekuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha umoja, mshikamno na utulivu katika nchi hiyo ya Kiarabu. ***
Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita Marekani ilishindwa katika vita vya baharini vilivyozishirikisha meli za kivita za Marekani na Vietnam ya Kaskazini katika Ghuba ya Tonkin inayopatikana kwenye Bahari ya China ya Kusini.
Mikwaruzano hiyo ya kijeshi iliipa Marekani kisingizio cha kuingia vitani moja kwa moja na Vietnam ya Kaskazini. Wakati huo Washington ilikuwa ikiiunga mkono kwa pande zote Vietnam ya Kusini dhidi ya ile ya Kaskazini. Wanajeshi wa Marekani waliingia vitani moja kwa moja kupigana dhidi ya Vietnam ya Kaskazini.