Jumatano, tarehe Pili Septemba, 2026
Leo ni Jumatano tarehe 20 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1448 Hijria mwafaka na tarehe Pili Septemba 2026.
Siku kama ya leo miaka 998 iliyopita yaani tareher 20 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka 450 Hijria, alifariki dunia Abu Tayyib Tabari, faqihi na mwandishi wa Kiislamu huko Baghdad.
Abu Tayyib alizaliwa mwaka 348 Hijria huko Amol, moja kati ya miji ya kaskazini mwa Iran. Tabari alifanya safari katika nchi mbalimbali kwa lengo la kutafuta elimu. Abu Tayyib Tabari, aliishi na kufundisha huko Baghdad ambapo alikuwa miongoni mwa maulamaa wakubwa za zama zake. Faqihi Tabari alikuwa hodari katika taaluma ya fasihi na utunzi wa mashairi.
Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu mbalimbali na miongoni mwa vitabu hivyo ni "Jawab fi al Sima'a" na "al Ghinaa wa al Ta'aliqatil Kubra fil Furu'u. ***
Siku kama ya leo miaka 225 iliyopita, baada ya vita kadhaa baina ya vikosi vya utawala wa Othmania na jeshi la Uingereza kwa upande mmoja na vikosi vya Ufaransa kwa upande mwingine, hatimaye Wafaransa walishindwa katika vita na kulazimika kuondoka kikamilifu nchini Misri.
Ikumbukwe kuwa, baada ya Napoleone Bonaparte kuikalia kwa mabavu ardhi ya Misri, Uingereza ambayo katika zama hizo ilikuwa ikihesabiwa kuwa hasimu na mshindani mkuu wa Ufaransa katika masuala ya kiuchumi na kijeshi, ilihisi maslahi yake yakiwa hatarini.
Ni kwa sababu hiyo ndio maana Uingereza ikaungana na utawala wa Othmania kwa shabaha ya kwenda kuitoa Ufaransa huko Misri na kuzuia jeshi la Ufaransa lisisonge mbele.
Katika siku kama ya leo miaka 160 iliyopita, William Rowan Hamilton mwanahisabati na mtaalamu mahiri wa elimu ya fizikia wa Ireland alifariki dunia.
Alizaliwa mwaka 1805 na kuonyesha kuwa mwerevu na mwenye kipaji cha hali ya juu tangu akiwa mtoto mdogo. Hamilton alisoma kwa ami yake aliyekuwa kasisi. Alipofikisha umri wa miaka 13, mwanafizikia huyo mtajika wa Ireland alikuwa tayari anazifahamu lugha kadhaa za kimataifa. Hadi anafikisha umri wa miaka 22 alikuwa tayari ni mwalimu katika elimu ya nujumu. ***
Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, nchi ya Vietnam ilipata uhuru. Vietnam ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Ufaransa katikati mwa karne ya 19.
Mwaka 1940 nchi hiyo ikadhibitiwa na Japan baada ya Ufaransa kushindwa na Ujerumani wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Vietnam iliendelea kuwa chini ya utawala na udhibiti wa Japan hadi pale Japan iliposalimu amri mwishoni mwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. ***
Tarehe Pili Septemba mwaka 1945, Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vilifikia tamati baada ya Japan kusalimu amri bila ya masharti yoyote.
Baada ya Japan kushindwa mfululizo na majeshi ya waitifaki, ililazimika kusalimu amri katika vita hivyo, hasa baada ya miji yake miwili mashuhuri ya Hiroshima na Nagasaki kushambuliwa na Marekani kwa mabomu ya atomiki.
Baada ya tukio hilo lililotokea miezi minne tu baada ya kusalimu amri Ujerumani, nchi waitifaki ziliikalia kwa mabavu Japan kwa mujibu wa Mkataba wa Potsdam na Generali wa Kimarekani, Douglas MacArthur, akachaguliwa kuwa kamanda mkuu huko Japan.
Mwaka 1951, nchi 49 duniani zilitiliana saini mkataba wa amani na Japan, na mwaka mmoja baadaye nchi hiyo kwa mara nyingine tena ikaanza kujitawala na kujiamulia mambo yake yenyewe. ***
Miaka 64 iliyopita katika siku kama hii ya leo kulingana na kalenda ya Hijria shamsia, yaani tarehe 11 Shahrivar 1341 tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.2 kwa kipimo cha rishta lilitikisa eneo la Buin Zahra, kaskazini magharibi mwa Iran.
Katika tetemeko hilo la kutisha, zaidi ya watu elfu 20 waliuawa na maelfu ya wengine walijeruhiwa. Kutokea kwa tetemeko hilo nyakati za usiku kuliwafanya watu wachache tu waweze kunusuru maisha yao. Katika tetemeko la ardhi la Buin Zahra, vijiji 120 vilitokomezwa kikamilifu na mamia ya nyumba ziliharibiwa vibaya.
Baada ya tukio hilo, bila kupoteza muda, watu wa Iran walipeleka misaada yao katika eneo hilo na kukimbilia kuwasaidia wananchi wenzao waliojeruhiwa. Buin Zahra ni eneo la matetemeko ya ardhi kwani mwaka 2013 lilipatwa na zilzala nyingine iliyoua watu wapatao 300.