Kwa nini Marekani inaogopa kuweka vikwazo dhidi ya nchi zinazoshirikiana na Iran?
Huku Marekani ikijaribu kuonyesha kuwa inatekeleza vita vikubwa zaidi vya kiuchumi dhidi ya Iran na kuanzisha mbwembwe zisizo na mfano wake katika uwanja huo, jambo linalojitokeza zaidi katika uhalisia wa mambo si taathira kubwa za vikwazo hivyo vinavyopigiwa debe, bali ni migongano na kuchanganyikiwa watawala wa Marekani kuhusu suala hilo.
Sakata la "Siku ya Uamuzi wa Kiuchumi" (Economic D-Day) au "operesheni kubwa ya mashambulizi ya kiuchumi dhidi ya Iran" limekejeliwa na Mohammad Bagher Ghalibaf, Spika wa Bunge la Iran, kuwa linatoa taswira ya wazi kuhusu hali ngumu na tata ambayo Marekani inajikuta ndani yake. Hii ni hali ambapo vitisho vya kujaribu kuyaadhibu mataifa yanayoshirikiana na Iran havitokani na nafasi ya nguvu, bali na hofu na kukata tamaa.
Scott Bessent, Waziri wa Fedha wa Marekani ambaye awali alikuwa amefananisha vikwazo vipya dhidi ya Iran na tukio kubwa la kutua kwa majeshi huko Normandy wakati wa Vita vya Pili vya Dunia katika makala ya gazeti la Financial Times, alikabiliwa na swali katika mkutano na waandishi wa habari siku iliyofuata kuhusu udhaifu na kutokuwa na mashiko kwa madai hayo. Kwa mshangao wa wote, alijibu kwa kusema: "kwani, ninataka kulipua uchumi wa dunia?!" Hatua hii ya wazi ya kulegeza msimamo ilikabiliwa na kejeli ya Ghalibaf kwenye mtandao wa X ambaye alisema: "Mpango huu haukufanana hata kidogo na tukio la kutua askari huko Normandy bali ulikuwa kama onyesho la mzaha wa kijinga klabuni ambapo mwigizaji alisahau hata mistari yake ya kuchekesha hadhira."
Mbali na hayo, kuna sababu muhimu zinazofanya Marekani iogope kuweka vikwazo dhidi ya nchi zinazokataa kujiunga na vikwazo vipya dhidi ya Iran. Marekani imepanua wigo wa vikwazo vyake vya ngazi ya pili ili kujumuisha sekta tano muhimu; rasilimali za kidijitali, teknolojia, dhahabu, usafiri wa anga na wa baharini, huku ikiweka vikwazo 60 zaidi dhidi ya taasisi, watu binafsi na mashirika ya meli. Kwa mujibu wa Bessent, lengo la kampeni hiyo ni "kukata njia zote muhimu za kiuchumi zinazoiimarisha Jamhuri ya Kiislamu, na kuiacha Tehran ikiwa imetengwa kabisa."
Pamoja na hayo, Washington inafahamu vizuri kuwa vitisho hivi vinakabiliwa na kikwazo kikubwa: Dunia ya leo imejengeka katika mifumo tata ya mahusiano na utegemezi wa kiuchumi, ambayo haiwezi kuvunjwa kirahisi kupitia amri ya Marekani. Nchi kama vile China, Uturuki, na Falme za Kiarabu (UAE) ni miongoni mwa washirika wakubwa wa kibiashara wa Iran. Vikwazo vya aina hii si tu kwamba vinaweza kuvuruga mfumo wa uchumi wa dunia, bali pia vinaweza kuweka gharama kubwa kwa uchumi wa Marekani na washirika wake. Marekani inafahamu vyema kwamba kuwawekea vikwazo vya ziada washirika wa kibiashara wa Iran kunaweza kusababisha vita kamili vya kiuchumi vyenye madhara ya kimataifa yasiyoweza kudhibitiwa.
Aidha, uzoefu wa kihistoria unaonyesha kuwa vikwazo vya upande mmoja vilivyowekwa na Marekani katika miongo kadhaa iliyopita si tu havijafanikiwa kufikia malengo, bali pia vimesukuma mataifa yaliyolengwa kutafuta njia mbadala za kushiriki katika uchumi wa dunia. Katika muktadha huu, mataifa yasiyo ya Magharibi, hasa yenye uchumi mkubwa kama China na Russia, yamekuwa yakitafuta kila mara kuepuka udhibiti wa dola na vikwazo vya Marekani kupitia mifumo kama vile kupanua kwa kiasi kikubwa kiwango cha ubadilishaji wa kiuchumi na biashara, kukuza ushirikiano wa fedha wa pande mbili, na kupunguza akiba yao ya fedha za kigeni inayotokana na dola. Washington inajua vizuri kwamba hatua zozote za kuziadhibu nchi hizi zinaweza kukabiliwa na vitendo vya kulipiza kisasi na kupelekea kuundwa kambi mpya za kiuchumi ambapo ushawishi na nguvu ya Marekani itapungua sana.
Jambo jingine muhimu ni wasiwasi wa Marekani kuhusu athari za kisiasa za hatua hizo. Esmaeil Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, amesema kuhusiana na vitisho hivyo kwamba: "Wakati mnyanyasaji anapotangaza kuwa kila benki, kampuni, bandari, na serikali lazima ichague kati ya kutii Washington na kukabiliwa na hatua za kulipiza kisasi za Marekani, suala hilo huwa halihusu tena Iran pekee." Kauli hii inaonyesha wazi kuwa tishio la kuiwekea vikwazo nchi ya tatu si hatua ya kiuchumi tu, bali ni changamoto kubwa kwa mamlaka ya kitaifa na uhuru wa kisiasa wa mataifa yanayolengwa. Nchi nyingi hasa zile za Asia Kusini zinaona vitendo hivi kama aina fulani ya "ugaidi wa kiuchumi" hivyo haziko tayari kufumbia macho uhuru wao kirahisi mkabala wa vitisho vya Washington.
Kusita Marekani kutekeleza vitisho vyake dhidi ya mataifa mengine, kunatokana na ukweli kwamba vikwazo vinapoteza taratibu taathira zake. Katika miongo minne iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kudumisha uchumi wake licha ya mashinikizo makubwa yasiyo na mfano wake ya nchi za Magharibi, kwa kutegemea "uchumi wa muqawama" (resistance economy), kupanua wigo wa washirika wake wa kibiashara na kupunguza utegemezi wake kwa dola. Aidha, mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iran yameshindwa kuvunja azma ya kisiasa ya Tehran ya kukabiliana na mashinikizo hayo. Hivyo, Washington inajikuta katika hali ngumu ambapo haina nguvu za kijeshi za kuilazimisha Iran isalimu amri, wala uhakika kwamba vikwazo kamili vya kiuchumi vitafanikiwa kuipigisha magoti.
Majibu ya kejeli ya Ghalibaf na maafisa wengine wa Iran kuhusiana na kauli hizo yanaakisi uhalisia uliopo: Marekani imenasa kwenye mtego ilioutega yenyewe. Kwa upande mmoja, inahisi kulazimika kutumia vitisho na maneno makali ili kulinda heshima yake; kwa upande mwingine, inaogopa madhara ya kivitendo yanayoweza kutokana na vitisho hivyovyo. Tukio lililotokea katika mkutano wa Bessent na waandishi wa habari, tukitumia maneno ya Ghalibaf, halikuwa "Siku ya Ushindi" bali "Siku ya Mchekeshaji"; siku ambayo mwigizaji mkuu si tu alisahau mistari ya uchekeshaji wake, bali pia alidhihirishia hadhira ya kimataifa kuwa yale yalikuwa maigizo matupu yasiyo na uhalisia. Mpango wa "kutengwa kiuchumi" unaweza kuonekana kuwa ni wa kuvutia sana kwenye karatasi na katika vyombo vya habari, lakini kiuhalisia, unaashiria hatua za mwisho za mkakati ulioshindwa, mkakati ambao, kutokana na hofu ya kufedheheka, umejikuta katika hali ya kujidhuru wenyewe.