Umoja wa Afrika walaani hatua za kuvuruga amani nchini Niger
-
Mahmoud Ali Youssouf
Umoja wa Afrika (AU) umelaani jaribio la uasi wa kijeshi lililozimwa NCHINI Niger. Mwenyekiti wa Kamisheni ya umoja huo Mahmoud Ali Youssouf ameikosoa hatua hiyo na kuonya dhidi ya hatua yoyote ya kuchukua madaraka kwa kutumia nguvu.
Katika taarifa yake, Mahmoud Ali Youssouf amesema amekuwa akifuatilia kwa karibu mapigano yaliyotokea katika maeneo ya mji mkuu Niamey huku akisisitiza kuwa, matumizi ya nguvu na vitendo vya kuvuruga utulivu wa taifa havipaswi kuvumiliwa, akitoa wito kwa pande zote kujizuia na kulinda usalama wa wananchi pamoja na uthabiti wa nchi.
Mji mkuu wa Niger, Niamey, ulirejea katika hali ya utulivu Jumapili iliyopita baada ya takriban saa 24 za mapigano yaliyoutikisa utawala wa kijeshi wa nchi hiyo. Wanajeshi waliokuwa na malalamiko dhidi ya serikali waliasi na kupambana na vikosi vilivyo waaminifu kwa kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdourahamane Tchiani.
Uasi huo umetajwa kuwa mojawapo ya vitisho vikubwa zaidi kwa serikali ya kijeshi tangu ilipotwaa madaraka kwa mapinduzi ya Julai 2023. Mapigano makali yaliendelea kuanzia usiku wa kuamkia Jumamosi hadi mwishoni mwa siku hiyo, huku milio ya risasi na milipuko ikisikika katika maeneo muhimu ya mji mkuu.
Niger imekuwa chini ya utawala wa Jenerali Abdourahamane Tiani tangu mapinduzi ya Julai mwaka 2023 yaliyomuondoa madarakani rais aliyechaguliwa kwa njia ya demokrasia Mohamed Bazoum, ambaye bado anazuiliwa hadi sasa.
Bazoum, mwenye umri wa miaka 66, amekuwa chini ya ulinzi mkali katika makazi ya rais mjini Niamey tangu mapinduzi ya Julai 2023. Licha ya kukaa kizuizini kwa zaidi ya miaka miwili, Bazoum hajawahi kutangaza kujiuzulu na anaendelea kujitambulisha kama rais halali wa Niger.
Alikuwa rais wa kwanza nchini humo kuingia madarakani kupitia uhamisho wa mamlaka kwa njia ya kidemokrasia kutoka kwa rais mmoja aliyechaguliwa hadi mwingine. Hata hivyo, Julai 26, 2023, serikali yake iliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya jeshi yaliyoongozwa na Jenerali Abdourahamane Tiani.