Mpango wa Chakula Duniani: Wapalestina 200,000 wamenyimwa msaada wa chakula
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141160-mpango_wa_chakula_duniani_wapalestina_200_000_wamenyimwa_msaada_wa_chakula
Mpango wa Chakula Duniani (WFP) sambamba na kuonya kuhusu kunyimwa Wapalestina 200,000 msaada wa chakula, umetahadharisha pia kuhusu mgogoro wa kiuchumi, ukosefu wa usalama wa chakula na kuzorota hali ya afya katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza.
(last modified 2026-09-03T03:22:51+00:00 )
Sep 03, 2026 03:21 UTC
  • Mpango wa Chakula Duniani: Wapalestina 200,000 wamenyimwa msaada wa chakula

Mpango wa Chakula Duniani (WFP) sambamba na kuonya kuhusu kunyimwa Wapalestina 200,000 msaada wa chakula, umetahadharisha pia kuhusu mgogoro wa kiuchumi, ukosefu wa usalama wa chakula na kuzorota hali ya afya katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza.

Mpango wa Chakula Duniani umetangaza kuwa, misaada kwa familia katika Ukingo wa Magharibi imepunguzwa kwa 50% kutokana na uhaba wa fedha. Kutokana na hali hiyo, msaada wa chakula kwa takribani Wapalestina 200,000 umesitishwa, huku mahitaji ya kibinadamu yakiwa yameongezeka mara mbili katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Shaun Hughes, Mkurugenzi wa Mpango wa Chakula Duniani huko Palestina, amesema kuwa kuongezeka mashambulizi ya walowezi wa Kizayuni na operesheni za kijeshi za utawala wa Kizayuni, sambamba na mgogoro wa kiuchumi na kuongezeka kwa ukosefu wa ajira, kumezidisha ukosefu wa usalama wa chakula.

Ameongeza kuwa theluthi moja ya wakazi wa Ukingo wa Magharibi wanakabiliwa na matatizo ya kupata mahitaji yao ya msingi.

Mpango wa Chakula Duniani pia umetangaza kuwa msaada wa fedha taslimu unaotolewa na taasisi hiyo katika Ukanda wa Gaza ulipunguzwa mwezi Julai uliopita kwa takribani familia 75,000.

Taasisi hiyo imeonya kuwa iwapo misaada ya kibinadamu haitaendelea kutolewa, kufikia mwisho wa mwaka huu huenda karibu 90% ya wakazi wa Ukanda wa Gaza wakakabiliwa na viwango vya juu vya ukosefu mkubwa wa usalama wa chakula.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa umesisitiza tena umuhimu wa kuwalinda raia na miundombinu ya Ukanda wa Gaza, ukisema kuwa takribani theluthi mbili ya familia katika eneo hilo wanaishi katika mahema au makazi ya muda, hali ambayo huzidi kuwa mbaya kwa kasi kutokana na mazingira magumu ya hewa.